May 25, 2024 06:08 UTC
  • Ujumbe unaotokana na kuwepo kwa wingi viongozi wa kigeni mjini Tehran kwa ajili ya kutoa heshima zao za mwisho kwa marehemu rais wa Iran

Viongozi wa nchi 68 na mashirika ya kieneo na kimataifa wametoa heshima zao za mwisho mjini Tehran kwa rais aliyeuawa shahidi akiwa na waziri wa mambo ya nje pamoja na viongozi wengine kwenye ajali ya helikopta iliyotokea kaskazini magharibi mwa nchi siku ya Jumapili.

Moja ya matukio machungu zaidi katika uwanja wa kisiasa wa Iran ni ajali ya helikopta iliyokuwa imembeba Sayyid Rais Ebrahim Raisi, Hossein Amirabdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje, Sayyid Mohammad Ali Aal Hashem, Imamu wa Swala ya Ijumaa wa Tabriz, Malik Rahmati, Gavana wa Azabajani Mashariki, pamoja na wahudumu wa ndege na walinzi wanne wa rais ambao wote walikufa shahidi katika ajali hiyo. Siku ya Jumatano, shughuli ya mazishi ya kuiaga miili mitukufu ya mashahidi hao ilifanyika, ambapo Jumatano hiyo hiyo jioni kulifanyika marasimu ya viongozi wa kigeni kwa ajili ya kutoa heshima zao za mwisho kwa miili ya Rais na Waziri wake wa Mashauri ya Kigeni katika Ukumbi wa Kikao cha Viongozi mjini Tehran.

Viongozi, maafisa wakuu wa nchi na wa mashirika ya kikanda na kimataifa wapatao 68 walihudhuria Marasimu hayo na kutoa heshima zao za mwisho kwa rais na wenzake waliouawa shahidi katika ajali hiyo ya kusikitisha. Aidha, kufikia sasa, mabalozi na wanadiplomasia wa nchi 50, baadhi ya maafisa wa Umoja wa Mataifa, mkuu wa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande wowote (NAM) na mkuu wa Kundi la 77 pamoja na China, wasomi, wawakilishi wa mashirika ya kiraia na wawakilishi wa vyombo vya habari, wamefika na kutia saini kitabu cha kumbukumbu katika Ofisi ya Uwakilishi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kutoa heshima zao za mwisho kufuatia kifo cha Rais na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran.

Katika nchi nyingi, viongozi wamefika katika balozi za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kutia saini kitabu cha kumbukumbu kwa shabaha ya kutoa heshima zao za mwisho kwa hayati Rais na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran.

Kiwango hiki cha mahudhurio na kutoa heshima kwa rais aliyeuawa shahidi wa Iran na waziri wake wa mambo ya nje kina nukta kadhaa muhimu za kuzingatiwa.

Viongozi wa kigeni wakitia saini kitabu cha kumbukumbu kufuatia kifo cha Rais Rais na Waziri wake wa Mambo ya Nje

Jambo la kwanza ni kwamba, katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wao, Rais Ebrahim Raisi na Hossein Amirabdollahian wamefanikiwa pakubwa kuakisi sura nzuri ya amani na chanya ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa nchi za dunia hususan za eneo la Asia Magharibi. Safari ya Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Bahrain mjini Tehran, licha ya kutokuwepo uhusiano wa kidiplomasia baina ya nchi mbili, na pia uwepo wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri mjini Tehran, ambayo ilikuwa safari yake ya kwanza nchini, ni jambo linaloashiria mafanikio hayo muhimu ya serikali ya 13 iliyoongozwa na Ebrahim Raisi.

Jambo la pili ni kuwa salamu nyingi za rambirambi kwa Rais na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran ni dalili ya wazi inayoonyesha kushindwa kwa stratijia ya Marekani ya kutaka kuitenga Iran. Kuhusiana na hilo, tovuti ya Marekani ya Bloomberg imeandika katika ripoti yake kwamba, kuwepo kwa wingi viongozi wa kigeni katika mazishi ya Rais Raisi kunaashiria kushindwa kwa juhudi za Marekani za kuitenga Iran. Katika ripoti hiyo ya uchambuzi, Bloomberg imeandika kuwa idadi kubwa ya viongozi wa nchi za nje walioshiriki katika mazishi ya kuuaga mwili wa marehemu Raisi inaashiria mafanikio ya Iran katika kuvunja vikwazo vya Marekani na kuboresha uhusiano na majirani zake.

Jambo la tatu ni kwamba huku utawala wa kibaguzi wa Israel ukiendelea kuchukiwa na kutengwa katika ngazi za kimataifa, na suala hilo kufikiwa kiwango cha juu zaidi katika historia yake, serikali ya 13 ya Rais Raisi imefanikiwa pakubwa kuvunja stratijia ya Marekani ya kueneza chuki dhidi ya Iran katika ngazi za kimataifa na hivyo kunyanyua nafasi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kieneo na kimataifa. Kukasirishwa watawala wa Tel Aviv na mahudhurio hayo makubwa ya viongozi wa dunia katika mazishi ya Raisi na vilevile kutumwa salama za rambirambi kufuatia kifo chake na cha waziri wake wa mambo ya nje ni uthibitisho wa wazi kuhusu ukweli huo. Gilad Erdan, balozi na mwakilishi wa kudumu wa Israel katika Umoja wa Mataifa siku ya Jumatatu alitoa matamshi ya matusi na kuwakejeli wanachama wa Baraza la Usalama kwa kusema: "Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo limenyamaza kimya kwa dakika moja kwa ajili ya kumkumbuka Rais wa Iran!" Balozi huyo wa utawala ghasibu wa Israel aliendelea kuhoji: "Ni hatua gani nyingine itakayochukuliwa na Baraza la Usalama? Dakika moja ya kimya kwa ajili ya kumbukumbu ya kila mwaka!"