Jun 16, 2024 02:42 UTC
  • Kambi ya kijeshi ya Israel yateketea kwa moto baada ya kushambuliwa na HAMAS

Duru za habari zimetangaza kuwa, kambi moja ya kijeshi ya utawala wa Kizayuni karibu na Ukanda wa Ghaza imeteketea kwa moto baada ya kushambuliwa na wanamapambano wa Izzuddin al Qassam, Tawi la Kijeshi la Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS.

Kwa mujibu wa Iran Press, Brigedi za Izzuddin al Qassam zimeshambulia kambi ya kijeshi ya Kissufim ya utawala wa Kizayuni wa Israel karibu na Ukanda wa Ghaza.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Kizayuni, shambulizi la makombora la HAMAS dhidi ya kambi hiyo limesababisha kuwaka moto maeneo yake.

Vyombo hivyo vya habari vya Kizayuni vimetangaza pia habari ya kuendelea kuwaka moto mkubwa katika maeneo ya kaskazini mwa ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni kutokana na mashambulizi ya Hizbullah ya Lebanon na hadi tunaripoti habari hii, maeneo hayo ya Wazayuni yalikuwa yanaendelea kuteketea kwa moto.

Kwa miezi kadhaa sasa Hizbullah ya Lebanon imekuwa ikishambulia maeneo tofauti ya kijeshi ya utawala wa Kizayuni kutokana na Israel kufanya jinai kubwa na za kutisha mno dhidi ya wananchi wasio na hatia wa Palestina hasa wa Ukanda wa Ghaza.

Hadi hivi sasa makumi ya maelfu ya Wazayni wamekimbia kutoka kwenye vitongoji vya walowezi wa Kizayuni vilivyoko karibu na mpaka wa Lebanon kwa kuhofia mashambulizi ya Hizbullah.

Tags