Jun 16, 2024 03:00 UTC
  • Walinzi wa mpaka wa Iran wazima njama za shambulio la kigaidi kabla ya uchaguzi wa rais wa mapema

Kamanda wa polisi wa mpakani wa Iran anasema kuwa, vikosi vyake vimetibua njama ya kigaidi kabla ya uchaguzi wa rais wa Juni 28, na kuwalazimisha magaidi hao waliopanga kufanya mashambulio ndani ya Iran kuikimbia nchi na kuacha nyuma silaha zao.

Brigedia Jenerali Ahmad Ali Goudarzi alisema hayo jana Jumamosi na kuongeza kwamba operesheni hiyo ya kukabiliana na ugaidi ilifanywa katika mkoa wa kusini mashariki mwa Iran yaani Sistan na Baluchestan karibu na mpaka na Pakistan.

Amesema magaidi hao walikuwa wanajaribu kujipenyeza ndani ya ardhi ya Iran kupitia mpaka wa Kaunti ya Saravan lakini waligunduliwa na njama zao kutibuliwa kutokana na umakini na ufuatiliaji wa karibu wa walinzi wa mpakani wa Iran.

Ameongeza kwa kusema: "Vikosi vya ulinzi vya Iran vilikabiliana na magaidi hao kwa kurushiana risasi vikali na kuwaacha wengi wa magaidi hao wakiwa wamejeruhiwa na kuwalazimisha hatimaye kuikimbia nchi."

Kiwango kikubwa cha silaha, ikiwa ni pamoja na mada za miripuko fuse za kielektroniki, risasi na katuni za bunduki aina ya AK-47, maguruneti yaliyotengenezwa Marekani na radio-call zimekamatwa na vikosi vya ulinzi vya Iran kwenye Operesheni hiyo.

Jenerali Goudarzi aidha amesisitiza kuwa, walinzi wa mpakani wa Iran hawatasita kukabiliana vilivyo na genge lolote la kigaidi linalojaribu kuingia humu nchini kinyemela ili kufanya ugaidi.

Tags