Jun 15, 2024 11:25 UTC
  • Rais wa Brazil alaani jinai za utawala wa Kizayuni Israel Gaza

Rais Luiz Inacio Lula da Silva wa Brazil amesema kuwa, haki ya kujihami inayodaiwa na utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukanda wa Gaza imegeuka na kuwa haki ya kulipiza kisasi katika kivuli cha ukiukwaji wa kila siku wa sheria na haki binadamu.

Da Silva amesema hayo wakati wa hotuba yake katika mkutano wa G7 na kueleza kwamba, ukiukaji wa kila siku wa sheria na haki za binadamu ambao umegharimu maisha ya maelfu ya raia wasio na hatia huko Gaza, ilitusukuma kuunga mkono uamuzi wa Afrika Kusini wa kuishtaki Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ).

Hayo yanajiri katika hali ambayo, kamati ya kutafuta ukweli ya Umoja wa Mataifa imetangaza kuwa, utawala unaokalia kwa mabavu wa Quds umefanya "maangamizi" ya Wapalestina wakati wa vita dhidi ya Ukanda wa Gaza.

Ripoti ya tume hiyo inaeleza kuwa, mauaji dhidi ya Wapalestina, kuteswa kwa misingi ya jinsia dhidi ya wanaume na wavulana wa Kipalestina, kulazimika kuyahama makazi yao, mateso na ukatili wa kinyama dhidi ya Wapalestina ni miongoni mwa jinai nyingine zinazofanywa na utawala wa Kizayuni katika vita vya Ukanda wa Gaza.

Utawala wa Kizayuni umeshtakiwa na unashutumiwa kwa mauaji ya kimbari katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ, ambayo uamuzi wake wa hivi karibuni umeiamuru Tel Aviv isitishe mara moja operesheni yake ya kijeshi katika mji wa kusini wa Rafah, ambako zaidi ya Wapalestina milioni moja walikimbilia kutafuta hifadhi kutokana na vita kabla ya mji huo nao kuvamiwa Mei 6.