Jun 16, 2024 06:03 UTC
  • Jeshi la Marekani liliendesha kampeni ya siri dhidi ya China wakati wa janga la UVIKO-19

Shirika la habari la Reuters la nchini Uingereza limeripoti kuwa, jeshi la Marekani liliendesha operesheni ya siri ya kisaikolojia ili kuidhoofisha China wakati wa janga la UVIKO-19.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya jana Jumamosi ya Reuters, wakati janga la UVIKO-19 lilipokuwa limepamba moto mwaka 2020, jeshi la Marekani lilianzisha operesheni ya siri ya kudhibiti na kugeuza kile ilichokiona kuwa tishio la Wachina linalotokana na kuongezeka nguvu za Beijing nchini Ufilipino.

Ufilipino ilikuwa miongoni mwa mataifa yaliyoathiriwa zaidi na virusi hatari vya corona.

Ili kuidhoofisha China, Wamarekani walizindua kampeni ya kueneza habari za uongo huko Ufilipino, wakidai kuwa Wachina hawakuendeleza na kueneza virusi tu lakini pia walikuwa wakitoa barakoa za bei nafuu na chanjo bandia kwa mataifa mengine ili ipate ushawishi wa kijiografia.

Amma kwa upande wake, Shirika la Utangazaji la Australia limetangaza kuwa, jeshi la Marekani lilikuwa limeanzisha kampeni kubwa dhidi ya Beijing kupitia akaunti bandia za mitandao ya kijamii ambazo zilikuwa zikieneza habari za uongo na kujifanya kama ni Wafilipino halisi.

Moja ya machapisho yaliyoenea sana wakati huo kwenye mitandao ya kijamii ilisema: "COVID imetoka China na CHANJO pia imetoka China, usiiamini China!" Hayo yalienea kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter kuanzia mwezi Julai 2020. 

Shirika la habari la Uingereza la Reuters limesema kwenye ripoti yake kwamba, kulitengenezwa mamia ya akaunti bandia kwenye mtandao wa X yaani Twitter ya zamani ili kueneza propaganda za uongo kuhusu corona au UVIKO-19.