Jun 15, 2024 11:31 UTC
  • Ayatullah Khamenei: Tangazo la kujibari na washirikina ni kubwa zaidi mwaka huu

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria jinai zinazofanywa na utawala katili na unaoelekea kusambaratika wa Israel huko Gaza na kusema: Suala la kujibari na kutangaza hasira dhidi ya washirikina ni kubwa zaidi mwaka huu kuliko huko nyuma.

Amesema hilo ni kwa sababu maafa ya Gaza hayajaacha nafasi ya kuzembea na kupuuza kadhia hiyo kwa mtu yeyote, chama, serikali na madhehebu yoyote ya Waislamu; na hali hii ya kujibari na kuchukizwa na washirikina inapaswa kudhihirishwa katika maneno na vitendo vya mataifa na serikali na kuzidisha mbinyo kwa wauaji na waungaji mkono wao.

Ayatullah Alii Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema hayo katika ujumbe kwa mahujaji wa Nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu wanaotekeleza ibada ya Hija ambapo ameutaja " Wito mzuri wa Ibrahim, ambao katika zama zote unawaita watu wote kwenye Al-Kaaba wakati wa msimu wa Hija, mwaka huu pia umevutia nyoyo za Waislamu kote duniani kwenye ngome ya Tauhidi na umoja. Amesema kujibari na tangazo la kujitenga na utawala ghasibu (Israel) na waungaji mkono wake, hususan Marekani, mwaka huu linapaswa kwenda mbali zaidi ya msimu wa Hija, na kuendelea katika nchi na miji mbalimbali ya Waislamu, katika maeneo yote ya dunia na kuwafikia watu wote. 2

Katika ujumbe huo, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, ameashiria vipengele vya ibada muhimu ya Hija akisema kuwa, vinatia nguvu katika nyoyo za Waislamu na kuwatia hofu na wahka watu wasiopenda mema.

Ayatullah Khamenei amesema: Qur’ani mbali na kueleza siri za muondo wa kina wa Hija, inaitaja kuwa ni dhihirisho la amani ya kimaadili na mapatano baina ya wa Waislamu, na kuwa vilevile kielelezo cha kuchukizwa na kusimama kidete dhidi ya maadui. Amesema mahujaji wanapaswa kukurubisha fikra na matendo yao kwa mafundisho haya yanayong'aa na warejee nyumbani na utambulisho mpya ulichanganywa na mafundisho hayo matukufu, kama tunu zenye thamani za safari ya Hija.

Mwishoni mwa ujumbe wake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amepongeza Muqawama na mapambano imara ya Palestina na watu wenye subira na madhulumu wa Gaza na kusisitiza kwamba, mapambano hayo yanapaswa kuungwa mkono kikamilifu.