Jun 16, 2024 06:34 UTC
  • Tovuti ya Kizayuni: Hizbullah inatumia akili mnemba katika droni zake

Tovuti ya Walla ya lugha ya Kiebrania imekiri katika ripoti yake mpya kabisa kwamba harakati ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon imeweza kupenya kwenye ukuta wa ulinzi wa jeshi la Israel kwa droni na ndege zake zisizo na rubani na kuchota taarifa za kijasusi.

Kwa mujibu wa shirika la habari la FARS, tovuti hiyo ya Kizayuni imesema katika ripoti yake ya jana Jumamosi kwamba Hizbullah ya Lebanon inapenya kila siku kwenye mifumo ya Israel kwa kutumia ndege zake zisizo na rubani.

Tovuti hiyo pia imeandika: "Hizbullah imeweza kupenya ukuta wa ulinzi wa Israel kwa kutumia akili-mnemba au Artificial Intelligence (AI) ndani ya aina zake mbalimbali za ndege zisizo na rubani na kuweza kuifikia miundombinu muhimu ndani ya Israel na kuishambulia."

Vile vile ripoti ya tovuti hiyo maarufu ya Kizayuni imeeleza kuwa, Hizbullah inaendelea kufanyia majaribio uwezo wake wa kijeshi mbele ya jeshi la Israel na kujiweka tayari kwa mapambano ya siku za usoni.

Tovuti hiyo ya Israel pia imesema: "Hizbullah ina uwezo wa kufanya shambulio kubwa kwa kutumia mamia ya ndege zisizo na rubani kwa mkupuo mmoja."

Kabla ya hapo Taasisi ya Usalama wa Ndani ya Israel nayo ilikuwa imekiri kwamba teknolojia ya droni na ndege zisizo na rubani za Hizbullah ni ya hali ya juu.

Ripoti hiyo iliyotolewa wiki iliyopita yaani tarehe 9 Juni ilisema pia kuwa, hivi sasa Hizbullah imeanza kutumia ndege zisizo na rubani ambazo zinaweza kurusha makombora na kukusanya taarifa kwa wakati mmoja.

Tags