Jun 15, 2024 11:28 UTC
  • Ripoti: Wanajeshi 10,000 wa Israel wameomba huduma za afya ya akili

Imeelezwa kwa akali wanajeshi 10,000 wa utawala haramu wa Israel wameripoti katika vituo vya matibabu na kuomba kupatiwa huduma ya afya ya akili.

Ripoti iliyochapishwa na gazeti la Israel la Jerusalem Post jana Ijumaa iliangazia hali "ya wasiwasi" wa afya ya akili inayowakabili wanajeshi vamizi wa Israel wanaorejea kutoka Ukanda wa Gaza.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa, kwa uchache wanajeshi 10,000 wa utawala haramu wa Israel wameripoti katika vituo vya matibabu na kuomba kupatiwa huduma ya afya ya akili.

Baadhi ya ripoti zinaeleza kwamba, mamia ya wanajeshi wa utawala haramu wa Israel wamekumbwa na maradhi ya akili tangu vilipoanza vita vya Gaza Oktoba mwaka jana (2023).

Gazeti la Kizayuni la Yedioth Ahronoth limeripoti kuwa, karibu asilimia 80 ya wanajeshi wa Israel waliokwenda kuomba matibabu ya akili kwenye vituo vya matibabu na mahospitali ya utawala wa Kizayuni wamo kwenye orodha ya majeruhi wa vita vya Ghaza.

Wakkati huo huo, tangu ilipoanza operesheni ya #Kimbunga_cha_al-Aqsa hadi hivi sasa, zaidi ya wakazi laki tatu wa utawala wa Kizayuni wameingia kwenye orodha ya watu wenye matatizo ya akili na saikolojia huko Israel.

Vituo vya matibabu ya akili vya Israel aidha vimesema kwenye barua yao kwamba, mfumo wa matibabu ya akili wa utawala wa Kizayauni umekaribia kusambaratika tena wakati huu ambapo kwa miaka kadhaa sasa vituo vya afya vya Israel vina matatizo ya bajeti na kukosekana wafanyakazi wa tiba na afya.