Wasiwasi wa Washington juu ya ushawishi wa Iran kati ya watetezi wa Palestina huko Marekani
(last modified Fri, 12 Jul 2024 10:41:23 GMT )
Jul 12, 2024 10:41 UTC
  • Wasiwasi wa Washington juu ya ushawishi wa Iran kati ya watetezi wa Palestina huko Marekani

Harakati ya wanafunzi wa vyuo vikuu nchini Marekani iliyotikisa maeneo yote ya hiyo na kusababisha mamia ya maandamano, mikusanyiko na migomo katika vyuo vikuu kulalamikia jinai na uhalifu wa Israel hususan mauaji ya kimbari ya watu wa Gaza imekabiliwa na hasira kali ya serikali ya Washington.

Sasa viongozi wa Marekani wanatoa matamshi ya kutaka kupotosha ukweli wa mambo ili kuonyesha kwamba harakati hiyo ya kupinga mauaji ya kimbari huko Gaza na kulaani ushiriki wa serikali ya Washington katika mauaji hayo imechochewa na nchi nyingine, hasa Iran.

Msemaji wa Ikulu ya White House, Karine Jean-Pierre, ameituhumu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa inatumia vibaya maandamano yanayohusiana na vita vya Gaza nchini Marekani na kusema kuwa, mwenendo huo haukubaliki. Msemajii wa White House amedai kuwa, uhuru wa kujieleza ni muhimu kwa demokrasia ya Marekani, lakini serikali pia ina wajibu wa kuwaonya raia kuhusu operesheni za ushawishi wa kigeni.

Matamshi hayo yametolewa saa chache baada ya Mkurugenzi wa Ujasusi wa Kitaifa wa Marekani, Avril Haines, kudai kuwa Iran inafanya hujuma za mtandaoni na kwamba mawakala wake wanatumia vibaya maandamano yanayofanyika dhidi ya Israel kuhusiana na vita vya Gaza. Avril Haines amesema katika taarifa yake kwamba: Marekani imewatambua waendeshaji mtandao wenye uhusiano na Iran ambao eti wanahamasisha maandamano na hata kutoa msaada wa kifedha kwa waandamanaji wanaopinga vita vya Gaza. Akiashiria ushahidi wake katika Bunge la Congress la Marekani, Mkurugenzi wa Ujasusi wa Kitaifa wa nchi hiyo amesema: "Iran inafanya jitihada za kueneza ushawishi wa kichokozi, kuzusha mifarakano na kudhoofisha imani kwa taasisi zetu za kidemokrasia."

Inaonekana kwamba, viongozi wa Marekani ambao wanakabiliwa na tukio la aina yake, yaani maandamano makubwa na yasiyo na kifani ya vijana wa Kimarekani hususan wanafunzi wa vyuo vikuu ya kupinga jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel katika vita vya Gaza, badala ya kuchunguza suala hili kwa undani, sasa wameamua kuzua madai ya uongo na kuituhumu Iran kuwa ndiyo inayochochea maandamano hayo. Haines amesisitiza katika madai yake ya ajabu kwamba, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inatafuta "fursa" katika maandamano yanayoendelea kupinga vita vya Gaza kwa kutumia "kitabu cha mwongozo" (Guidebook) ambacho kimetumiwa wengine kwa miaka mingi. Kwa maneno mengine tunaweza kusema kuwa, badala ya kushughulikia sababu halisi za kuanza vuguvugu la wanafunzi wa vyuo vikuu dhidi ya Israel huko Marekani, afisa huyu mkuu wa ujasusi wa serikali ya Washington anajaribu kuitambulisha Iran kama mwanzilishi wa harakati hiyo. Madai haya yanathibitika kutokuwa na  msingi wowote kwa kufanya uchunguzi mdogo kuhusu harakati hiyo iliyoenea katika vyuo vikuu vya Marekani na nchi nyingi za Magharibi.

Pamoja na haya yote, kuna masuala kadhaa yanayopaswa kuzingatiwa katika suala hili. Kwanza ni kwamba, katika dunia ya karne ya 21, ambayo ni karne ya mawasiliano na habari, anga ya intaneti na mitandao ya kijamii, na kwa kuzingatia maendeleo ya teknolojia mpya katika uwanja wa mawasiliano, ukiritimba wa habari na vyombo vya habari umeondolewa kwenye mikono ya Magharibi, haswa Marekani. Hii leo, nchi mbalimbali zinaweza kutoa maoni yao juu ya matukio ya kikanda na kimataifa katika ngazi mbalimbali duniani, kulingana na kiwango cha uwezo wao katika medani ya vyombo vya habari na shughuli zao katika anga ya mtandao. Hivyo basi, kutokana na mafanikio makubwa iliyoyapata katika nyanja za mawasiliano na anga za juu, Iran ina uwezo wa kueneza maoni na ujumbe wake katika maeneo mbalimbali za dunia, ikiwemo Marekani, ikitumia vyombo vyake vya habari, mtandao na satalaiti. Na kwa kuzingatia ujumbe wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran hususan misimamo na mitazamo ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei, idadi kubwa ya watu katika nchi mbalimbali wakiwemo vijana wa Marekani, wanatilia maanani jumbe hizo na kuzifuatilia.

Katika mkondo huo, barua ya hivi karibuni ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa wanafunzi wa vyuo vikuu wa Marekani, iliyochapishwa tarehe 30 Mei 2024, si uingiliaji wa masuala ya ndani ya Marekani, bali ni kuthamini na kutoa maelezo kuhusu harakati ya ndani ya Marekani iliyoanzishwa na wanafunzi wa vyuo vikuu wakiwatetea watu wanaodhulumiwa Palestina, na kulaani jinai zinazofanywa na utawala wa Kizayuni katika vita vya Gaza; na vilevile misaada na ushiriki wa serikali ya nchi yao katika mauaji ya kimbari ya Gaza. Iran haikuwa na nafasi yoyote katika kuanzisha harakati hiyo na imeeleza tu uungaji mkono wake kwa maandamano hayo katika fremu kutetea kadhia ya ukombozi wa Palestina, mwamko unaozidi kukua miongoni mwa vijana wa Kimagharibi hususan Wamarekani kuhusu Wapalestina, na ongezeko la chuki na hasira zao dhidi ya Israel.

Nukta muhimu ni kwamba maandamano ya wanafunzi nchini Marekani kuiunga mkono Palestina ni jambo jipya katika mfumo wa kisiasa na kijamii wa nchi hiyo. Maandamano makubwa yasiyo na kifani katika vyuo vikuu vya Marekani ya kuwaunga mkono Wapalestina na kupinga jinai na mauaji ya kimbari ya Israel, kwa mara nyingine tena yanaashiria mabadiliko ya kimsingi na muhimu katika mtazamo wa kizazi cha vijana wa Marekani na Magharibi kwa ujumla kuhusu suala la Palestina.

Kwa sasa kunajitokeza swali kwamba, kwa nini kizazi cha vijana, au kwa maneno mengine, "Gen Z", tofauti na baba zao, wanaiunga mkono Palestina na hawana huruma yoyote na utawala wa Kizayuni wa Israel?

Maafisa na taasisi zilizo karibu na lobi za Wazayuni huko Marekani, pamoja na viongozi wa serikali ya Tel Aviv, wanafanya jitihada za kupotosha ukweli wakidai kuwa maandamano na upinzani wa wanafunzi na wahadhiri wa vyuo vikuu ni matokeo ya kudanganywa na kupotoka kwa kizazi kipya cha Marekani, na wamevitaka vyombo vya usalama kuwashughulikia waungaji mkono wa Muqawama. Wanakanusha kwa makusudi uhakika kwamba, hiyo ni harakati ya iliyoibuka ndani ya Marekani kwenyewe kutokana na mabadiliko ya mtazamo wa vijana wa Marekani dhidi ya Israel kwa upande mmoja, na mshikamano na uungaji mkono wao kwa Wapalestina wanaofanyiwa ukatili wa kutisha kwa upande mwingine.