Russia: Tehran na Moscow zinaendelea kuyafanyia kazi makubaliano makubwa ya ushirikiano
Baada ya kuchapishwa taarifa kuhusu kusimamishwa kwa muda makubaliano ya ushirikiano kati ya Iran na Russia; Dmitry Peskov Msemaji wa Ikulu ya Russia (Kremlin) amesema kazi ya kutekeleza makubaliano makubwa kati ya nchi yake na Iran inaendelea lakini ratiba imebadilika kwa sababu ya kufanyika uchaguzi nchini Iran.
Katika hali ambayo baadhi ya vyombo vya habari viliripoti kuwa makubaliano ya muda mrefu kati ya Iran na Russia yamesitishwa kwa muda kwa kumnukuu Zamir Kabulov Mjumbe Maalumu wa Rais wa Russia katika masuala ya Afghanistan; Dmitry Peskov Msemaji wa Ikulu ya Russia na Maria Zakharova Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo wameashiria kunukuliwa kimakosa matamshi ya Kabulov na kusisitiza kuwa kazi ya kukamilisha makubaliano hayo inaendelea.
Wakati huo huo Kazem Jalali Balozi wa Iran nchini Russia amesema kuwa taarifa kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Russia zimesimamisha makubaliano ya ushirikiano kati yao ni ya uwongo.
Amesema Shahidi Hussein Amir Abdollahian Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alikuwa akifuatilia pakubwa suala hilo na mazungumzo ya mwisho aliyofanya naye ilikuwa ni kuhusu kusogeza jambo hilo katika marhala ya utiaji saini haraka iwezekanavyo.