Bagheri Kani: Uvamizi wa Wazayuni katika Msikiti wa Al-Aqsa unalenga kuzidisha mivutano
Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema uvamizi wa baadhi ya mawaziri wa serikali ya utawala bandia wa Israel na walowezi wa Kizayuni katika msikiti wa al Aqsa ni hatua ya kichochezi inayolenga kushadidisha mivutano na ukosefu wa amani katika eneo.
Ali Bagheri Kani amelani hatua za kichokozi za baadhi ya mawaziri wa serikali bandia ya Israel na walowezi wa Kizayuni katika msikiti wa al Aqsa na kusisitiza juu ya udharura wa kutolewa radiamali kimataifa hasa serikali za Kiislamu na mataifa ya Kiislamu katika uwanja huo.
Bagheri Kani ameongeza kuwa: Jamii ya kimataifa na taasisi za kimataifa zina wajibu wa wazi na wa dharura wa kuchukua hatua ili kusitishwa vitendo vya kinyama na ukiukaji wa haki za sheria na kanuni za kimataifa unaofanywa na utawala wa Kizayuni.
Kuhusiana na suala hilo, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia amelaani vikali uvamizi uliofanywa na mawaziri wawili wa utawala bandia wa Israel na baadhi ya walowezi wa Kizayuni kwa kuuvunjia heshima na kuingia katika msikiti wa al Aqsa na kusema hatua hizo za uchochezi ni mfano mwingine wa wazi wa irada ya Wazayuni ya kueneza mivutano na machafuko katika eneo.
Itamar ben Gvir Waziri wa Usalama wa Ndani wa serikali ya utawala bandia wa Israel jana usiku akiwa pamoja na kundi la walowezi wa Kizayuni walivamia msikiti wa al Aqsa. Waziri huyo mwenye misimamo mikali wa kizayuni pia ametaka kusitishwa mazungumzo ya kufikia mapatano ya kusimamisha vita Ukanda wa Gaza na ametaka kuendelea vita dhidi ya Gaza. Ametamka haya katika ujumbe alioutuma kwa njia ya video.
Shambulio la Waziri mwenye misimamo mikali ya utawala ghasibu wa Kizayuni dhidi ya Msikiti wa Al-Aqsa na kuvunjiwa heshima eneo hilo takatifu limekosolewa na kulaaniwa vikali na makundi ya Palestina na baadhi ya nchi za Kiislamu.