Iran: Baka la aibu la Mapinduzi ya kijeshi ya 1953 litabakia milele kwenye mapaji ya nyuso za US na UK
Aug 18, 2024 12:15 UTC
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema, baka la aibu la kuiondoa madarakani Serikali halali ya Iran iliyochaguliwa na wananchi, kupitia mapinduzi ya kijeshi ya tarehe 28 Mordad 1332 (Agosti 19, 1953) na la kuuhami Udikteta kisiasa, kiusalama na kijeshi litaendelea kubakia milele kwenye mapaji ya nyuso za tawala za Marekani na Uingereza.
Mnamo tarehe 28 Mordad 1332 iliyosadifiana na Agosti 19, 1953, vikosi kadhaa vya jeshi la utawala katili wa kifalme, kwa kushirikiana na Marekani na Uingereza, viliipindua serikali ya Waziri Mkuu Mohammad Mosaddegh na kumrejesha tena madarakani Mfalme Mohammad Reza Pahlavi.
Mapinduzi hayo ya kijeshi ya Agosti 1953 yaliyoongozwa na Marekani na Uingereza, ambayo yalipelekea kuangushwa serikali halali ya Iran ya wakati huo yanakumbusha kipindi nyeti na hasasi cha historia ya kisiasa ya Iran kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Nasser Kanani Chafi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameandika kwenye mtandao wa kijamii wa X kwamba utumwa, ukoloni, mapinduzi na uingiliaji wa kijeshi katika nchi zingine ni sehemu tu ya rekodi chafu na ya kuaibisha ya uingiliaji uliofanywa na Marekani na Uingereza duniani.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Iran ameongeza kuwa, yakiwa yana faili chafu kama hilo, Marekani na Uingereza sasa hivi zinatoa uungaji mkono usio na kikomo kwa utawala bandia na wa kibaguzi wa Israel na mauaji ya kimbari unayofanya katika ukanda wa Ghaza, na wakati huo huo zinajinadi kuwa ndio ndio wabeba bendera ya kutetea haki za binadamu na demokrasia!.../