Sep 08, 2024 07:01 UTC
  • Mrusha mkuki wa Iran katika Paralimpiki apokonywa dhahabu kwa kupeperusha bendera ya kidini

Mwanariadha wa Iran Beit Sayyah, ambaye alinyakua medali ya dhahabu na kuweka rekodi mpya ya Paralimpiki (Olimpiki ya Walemavu) katika kategoria ya F41 ya mchezo wa kurusha mkuki kwa wanaume amepokonywa dhahabu hiyo katika hatua iliyozua utata.

Katika uamuzi ambao umewashangaza wengi wakati wa michezo ya Paralimipiki ya Paris 2024 inayomalizika leo, Sayyah alinyang'anywa nishani yake kwa kuonyesha bendera ya kidini wakati wa sherehe ya ushindi wake Jumamosi.

Beit Sayyah alipata medali hiyo kwa kuvurumisha mkuki umbali wa mita 47.64, na kuvunja rekodi ya Paralimpiki kwa mafanikio makubwa.

Walakini, waandaaji wa Olimpiki ya Walemavu walisema "hakustahili" kuonyesha bendera iliyokuwa na jina la Ummul Baneen (SA), mamake Hadhrat Abal Fazal Abbas (AS), mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW). Kwa msingi huo mwanariadha huyo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amepokonywa medali yake kidhulma na nafasi yake  ikachukuliwa na Navdeep Singh wa India, ambaye awali alishinda fedha.

Tovuti rasmi ya Michezo ya Olimpiki ya Walemavu ya Paris ilisema mwanariadha huyo wa Iran alipatikana na hatia kwa "ukiukaji wa sheria za michezo."

Hata hivyo, wachambuzi wa michezo wanasema kwamba hatua hiyo si sahihi na ni sawa na kuingiza siasa katika Michezo ya Olimpiki kwa matakwa ya mamlaka ya Ufaransa ambayo ni mwenyeji wa mashindano ya michezo hiyo. Serikali ya Ufaransa imekuwa ikitekeleza sera za chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu kwa muda mrefu na hata imewapiga marufuku wanariadha wake Waislamu wa kike kuvaa Hijabu.

Ni vyema kuashiria hapa kwamba Sayyah alikuwa ameonyesha bendera hiyo hiyo katika Michezo ya Olimpiki ya Walemavu ya Tokyo 2020, ambapo alishinda medali ya fedha, bila kukabiliwa na hatua yoyote. ya chuki

Kikosi cha Iran katika Michezo ya Olimpiki ya Walemavu ya Paris kiliwasilisha pingamizi lao kali dhidi ya uamuzi huo, lakini limekataliwa.