Upeo angavu katika uhusiano wa Iran na Pakistan
(last modified Tue, 05 Nov 2024 07:50:29 GMT )
Nov 05, 2024 07:50 UTC
  • Upeo angavu katika uhusiano wa Iran na Pakistan

Sayyid Abbas Araghchi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran jioni ya jana Jumatatu aliwasili Islamabad, mji mkuu wa Pakistan kwa lengo la kukutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa ngazi za juu wa nchi hiyo na kushauriana nao kuhusu uhusiano wa pande mbili na matukio ya kieneo.

Ziara ya Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Pakistan inazidi kuonyesha kuweko upeo angavu katika kustawishwa uhusiano kati ya Tehran na Islamabad katika pande zote. Katika safari hii ya siku mbili, Araghchi anatarajiwa kujadili njia za kuendeleza zaidi uhusiano baina ya nchi hizo mbili na kujadili matukio ya kikanda katika mazungumzo kwa nyakati tofauti na Waziri Mkuu Shahbaz Sharif pamoja na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje Muhammad Is'haq Dar.

Kuakisiwa habari ya ziara ya Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Pakistan katika vyombo vya habari vya nchi hiyo kunaonyesha hadhi ya juu ya Iran mbele ya wananchi na viongozi wa serikali ya Pakistan, kiasi kwamba, vinaitathmini safari hii kama fursa muhimu sana ya kusukuma mbele gurudumu la ushirikiano na mazungumzo kati ya nchi hizo mbili katika nyanja mbalimbali zikiwemo za biashara, nishati na usalama.

Uhusiano kati ya Tehran na Islamabad uliingia katika hatua mpya katika serikali ya awamu ya 13 ya shahidi Ibrahim Raisi na mchakato huu wa kustawisha uhusiano huo unaendelea. Katika uwanja wa mahusiano baina ya nchi mbili, suala la kwanza ambalo linatiliwa mkazo mno na duru za kisiasa, kiuchumi na hata vyombo vya habari vya Pakistan ni nishati hususan gesi.

Sayyid Abbas Araghchi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran 

 

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilikubali kuiuzia gesi nchi hiyo kwa kuzingatia makubaliano yaliyotiwa saini na Rais wa Pakistan, Asif Ali Zardari, na kujenga bomba la kusafirisha nishati ya gesi hadi kwenye mpaka na Pakistan. Licha ya kigugumizi na hatua za kusitasita zilizoonyeshwa na serikali zilizopita nchini Pakistan, lakini serikali ya Shahbaz Sharif inasisitiza juu ya utekelezaji wake, ambao ukizingatiwa unaweza kukidhi mahitaji ya gesi ya Pakistani, haswa katika sekta ya viwanda na kudhamini mahitaji ya umeme.

Mbali na hayo mabadilishano ya kibiashara kati ya Iran na Pakistan si ya kuridhisha. Hii ni pamoja na kuwa, Iran na Pakistan zina uwezo mkubwa katika sekta zote za viwanda, ujenzi, kilimo, dawa na elimu. Kwa kuzingatia hayo inatarajiwa kuwa, muda si mrefu nchi hizo mbili zitaweza kuongeza kiwango cha mabadilishano ya kibiashara ya pande mbili na kufikia dola bilioni kumi likiwa ndilo lengo lililowekwa na nchi hizo. Kuhusiana na hili, kuimarishwa na kuendelezwa kwa soko za mpakani ni mambo yanayozingatiwa ma Tehran na Islamabad.

Suala la tatu muhimu katika mahusiano baina ya nchi mbili hizi ni usalama wa mipaka ya pamoja na kukabiliana na vitendo vya ugaidi. Ingawa serikali na jeshi la Pakistan daima wamekuwa wakiahidi kushirikiana katika kukabiliana na makundi ya kigaidi, lakini kuendelea harakati za kigaidi zinazofanywa na baadhi ya makundi likiwemo kundi linalojiita Jaish Al-Adl kwa kujipenyeza ndani ya ardhi ya Iran, kunaonyesha kuwa, ili kudhamini usalama kamili wa mipaka ya pamoja ya nchi mbili hizi kuna haja ya kuweko ushirikiano wa pamoja wa kijasusi na kiusalama kati ya vikosi vya walinzi wa mipaka ya Iran na Pakistan.

 

Kwa kuzingatia nafasi muhimu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Pakistan katika eneo na ulimwengu wa Kiislamu, bila shaka mashauriano kati ya nchi hizo mbili na kutekelezwa mikakati ya pamoja kunaweza kuwa na taathira chanya katika matukio ya kieneo na ulimwengu wa Kiislamu. Jinai za utawala wa Kizayuni wa wa Iisrael dhidi ya Gaza na Lebanon na mauaji ya kimbari ya utawala huo katika eneo la Magharibi mwa Asia yanayotekelezwa kwa uungaji mkono kamili wa Marekani, yamefanya kuweko ulazima wa fikra za pamoja na ushirikiano zaidi kati ya Tehran na Islamabad katika kukabiliana na mauaji ya kimbari ya utawala wa Kizayuni wa Israel.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeonyesha kivitendo kwamba inaunga mkono kikamilifu kadhia ya Palestina dhidi ya wavamizi wa Kizayuni, sera ambayo pia inazingatiwa na kuungwa mkono na  Pakistan. Pamoja na hayo Tehran inaamini kuwa, nchi zote za Kiislamu zinapaswa kusimama pamoja kukabiliana na watenda jinai hao wa Kizayuni ili ziweze kuzuia kuendelea jinai  za utawala haramu wa Israel huko Gaza, Lebanon na katika ulimwengu mzima wa Kiislamu.