Pezeshkian asisitiza Umoja wa Kitaifa kama ufunguo wa maendeleo
(last modified Thu, 09 Jan 2025 11:07:02 GMT )
Jan 09, 2025 11:07 UTC
  • Pezeshkian asisitiza Umoja wa Kitaifa kama ufunguo wa maendeleo

Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza umuhimu wa umoja wa kitaifa kama msingi wa sera ya utawala wake, akiangazia nafasi yake muhimu katika maendeleo ya nchi.

Rais Pezeshkian amesema hayo katika mkutano uliopewa jina la "Mazungumzo ya Kitaifa Kwa Ajili ya Umoja wa Kitaifa, na kusisitiza umuhimu wa kutekeleza haki na uadilifu katika jamii.

Pezeshkian amebainisha kwamba kufanya mambo kinyume na haki kunadhoofisha msingi wa haki ndani ya jamii.

Rais Pezeshkian amesisitiza dhamira ya serikali yake ya kuwatumikia wananchi na kuepuka vitendo vyovyote vinavyoweza kuonekana kuwa vya makabiliano au uonevu.

Kadhalika amesisitiza ulazima wa maafikiano ya kukuza umoja na mshikamano wa kitaifa, akitahadharisha dhidi ya madai ya kupindukia ambayo yanaweza kukiuka haki za wengine.

Aidha Daktari Pezeshkian ametahadharisha dhidi ya mifarakano inayotokana na ubinafsi na ubabe na kusema kuwa, hali ya mambo nchini haiendani na hadhi ya watu wa Iran.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameonyesha imani yake juu ya uwezekano wa maendeleo na akahimiza kuingiza mawazo haya kwa watu hususan vijana.

Kadhalika amesema, juhudi lazima zifanywe ili kufika kilele cha utawi na maendeleo na kwamba, vijana na wasomi na matabaka yote ya watu yanapaswa kushirikishwa na kuwa mstari wa mbele katika hilo.