CIA yakiri kwamba mradi wa nyuklia wa Iran ni wa amani
Mkuu wa shirika la kijasusi la Marekani (CIA) amekiri kwamba mradi wa nyuklia wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni wa kiraia na hakuna ushahidi wowote unaoonesha kuwa mradi huo umeelekea upande wa kijeshi.
William Burns amesema hayo katika mahojiano na redio ya NPR ya Marekani alipohojiwa kuhusu matukio ya hivi karibuni ya Asia Magharibi na amesema: "Hakuna dalili zozote zinazoonesha kuwa Iran imeamua kutengeneza silaha za nyuklia."
Aidha katika kujibu swali kuhusu matukio ya ukanda wa Asia Magharibi, Burns amedai kuwa eti nafasi ya kimkakati ya Iran imedhoofika kwenye eneo hilo.
Mkuu wa shirika la kijasusi la Marekani "CIA" ameendelea kutoa madai ya uongo kwamba Tehran huko nyuma ilikuwa inafanya juhudi za kumiliki silaha za nyuklia na kudai kuwa, mwaka 2003 Iran eti ilibadilisha msimamo wake wa kumiliki silaha za atomiki.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima imekuwa ikitilia mkazo kwamba haijawahi kuwa na nia ya kumiliki silaha za maangamizi ya umati zikiwemo za nyuklia kwani kwa mujibu wa itikadi zake za kidini, ni haramu kumiliki silaha za namna hiyo.
Mashirika mbalimbali ukiwemo Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA yamethitibisha katika ripoti zao nyingi rasmi na zisizo rasmi kwamba mradi wa nyuklia wa Iran ni wa kiraia na ni wa amani kikamilifu.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imesisitiza mara nyingi tu kuwa, mradi wa nyuklia wa Jamhuri ya Kiislamu unaendeshwa kwa mujibu wa sheria za kimataifa, chini ya uangalizi IAEA, uko wazi na haujawahi kwenda kinyume na malengo yake ya kiraia.