Kamanda Salami wa IRGC : Hatutasalimu amri mbele ya tishio lolote
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu IRGC amesema nguvu za Iran na historia yake pana inaifanya isiweze kutetereshwa na mashinikizo ya nje.
Meja Jenerali Hossein Salami amesema hayo kujibu hatua ya Marekani kuiwekea Iran vikwazo vipya na kuongeza kuwa, wakati mataifa yenye nguvu yanaweka vikwazo na njama za kudumaza ustawi na maendeleo ya Iran, lakini nchi hii imezidi kuimarika chini ya uongozi thabiti.
Salami ameeleza bayana kuwa, historia kongwe na ya jadi na nguvu za kipekee zinaifanya Iran kuwa taifa ambalo Marekani na washirika wake wanaona hawawezi kulivumilia.
Kauli ya Kamanda Salami inatia nguvu azma ya Iran ya kudumisha mamlaka yake ya kujitawala na uhuru wa kimkakati. Amesema Jamhuri ya Kiislamu itafuata njia yake ya uwezeshaji na ushirikiano bila kukubali kusalimu amri mbele ya vitisho vya maajinabi.
Wakati huo huo, Iran imelaani vikali vikwazo hivyo vipya vilivyowekwa na utawala wa Rais Donald Trump wa Marekani dhidi ya sekta ya mafuta ya nchi hii, ikisema vinaenda kinyume na sheria na kanuni za kimataifa.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Iran, Esmaeil Baghaei leo Ijumaa ameshutumu vikwazo hivyo na kusema kuwa "havifai kabisa". Matamshi hayo yametolewa siku moja baada ya Wizara ya Hazina ya Marekani kuwalenga zaidi ya watu 12, makampuni pamoja na vyombo vya baharini kwa madai kuwa vinarahisisha usafirishaji wa mamilioni ya mapipa ya mafuta ya Iran hadi China.
Vikwazo hivyo vilikuwa vya kwanza dhidi ya Iran baada ya Trump kuhuisha kampeni yake inayoitwa "mashinikizo ya juu zaidi" dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.
"Uamuzi wa utawala mpya wa Marekani wa kuliweka mashinikizo taifa la Iran kwa kuzuia biashara halali ya Iran na washirika wake wa kiuchumi, ni kitendo haramu, kilicho kinyume cha sheria na kisicho sahihi," Baghaei aliongeza. Amesema: Jamhuri ya Kiislamu itaibebesha dhima Marekani kwa matokeo hasi ya hatua hizo za upande mmoja za uonevu.