Pezeshkian: Iran inakaribisha kuhuishwa uhusiano wake na Sudan
(last modified Wed, 19 Feb 2025 12:11:16 GMT )
Feb 19, 2025 12:11 UTC
  • Pezeshkian: Iran inakaribisha kuhuishwa uhusiano wake na Sudan

Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian amesema Jamhuri ya Kiislamu inakaribisha kwa mikono miwili kurejeshwa kwa uhusiano wa nchi hii na Sudan, akisisitiza kuwa nchi za Kiislamu zinapaswa kuepuka mivutano na kukata uhusiano baina yao.

Rais Pezeshkian amesema hayo katika mazungumzo yake na Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan, Ali Youssef Ahmed Al-Sharif hapa mjini Tehran na kueleza kuwa,  "Hakuna sababu kwamba uhusiano kati ya nchi za Kiislamu unakuwa na mvutano na kukatika. Kwa sababu hiyo, tunakaribisha kuhuishwa uhusiano kati ya Iran na Sudan."

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza umuhimu wa kupanua mahusiano baina ya nchi hizi mbili katika nyanja mbali mbali.

Amesema Iran inatilia maanani uhusiano wake na Sudan, akielezea matumaini kwamba mataifa haya mawili yatafanya maamuzi mazuri katika suala hilo wakati kamisheni yao ya pamoja ya uchumi itakapofanya mkutano.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan kwa upande wake ameeleza kuridhishwa kwake na kurejeshwa uhusiano kati ya Tehran na Khartoum na kusema kuwa, nchi hiyo ya Kiafrika iko tayari kupanua zaidi uhusiano wake na Iran katika nyuga zote.

Ali Youssef Ahmed Al-Sharif amesema tume ya pamoja ya kiuchumi ya Iran na Sudan hivi karibuni itafanya kikao chake. Aidha amewasilisha salamu na ujumbe wa Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Sudan, Jenerali Abdel Fattah al-Burhan kwa Rais Pezeshkian.