Araghchi: IAEA inaweza kutatua kwa amani faili la nyuklia la Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i125292-araghchi_iaea_inaweza_kutatua_kwa_amani_faili_la_nyuklia_la_iran
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Sayyid Abbas Araghchi amesema Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) unaweza kuwa na nafasi na jukumu muhimu katika utatuzi wa amani wa suala la nyuklia la Jamhuri ya Kiislamu.
(last modified 2026-03-17T04:36:21+00:00 )
Apr 17, 2025 09:29 UTC
  • Araghchi: IAEA inaweza kutatua kwa amani faili la nyuklia la Iran

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Sayyid Abbas Araghchi amesema Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) unaweza kuwa na nafasi na jukumu muhimu katika utatuzi wa amani wa suala la nyuklia la Jamhuri ya Kiislamu.

Katika ujumbe aliotuma kwenye akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa X leo Alkhamisi, Araghchi amesema amefanya mazungumzo "ya manufaa" na Mkurugenzi Mkuu wa IAEA, Rafael Grossi mjini Tehran jana Jumatano.

"Wakati waharibifu mbalimbali wanakusanywa ili kuvuruga mazungumzo ya sasa, tunahitaji Mkurugenzi Mkuu wa Amani," ameongeza. Amesisitiza kuwa, "muelekeo" wa Iran ni kumwamini Mkuu wa Shirika la Nyuklia la Umoja wa Mataifa katika dhamira yake ya kuiweka IAEA mbali na siasa na kuendelea kuzingatia majukumu yake ya kiufundi.

Ujumbe wa Araghchi unakuja baada ya mkutano wake na Mkuu wa IAEA, ambaye yuko Tehran, na kabla ya duru mpya ya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani.

Katika kikao chake na Grossi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran kwa mara nyingine tena ameitaka IAEA ichukue msimamo wa wazi kuhusiana na vitisho ambavyo vimekuwa vikitolewa na pande mbalimbali dhidi ya vituo vya amani vya nyuklia vya nchi hiyo.

Araghchi amesema Iran imesalia na dhamira ya dhati ya kushirikiana kikamilifu na IAEA ndani ya majukumu yake ya kisheria ya kimataifa, lakini akasisitiza kuwa wakala huo pia unapaswa kuzingatia majukumu yake ya kiufundi na kitaaluma bila kuathiriwa na mashinikizo ya nje ya nchi.

Mkutano kati ya mwanadiplomasia huyo mkuu wa Iran na Grossi umefanyika huku kukiwa na vitisho vipya vya Israel vya kushambulia miundombinu ya nyuklia ya Jamhuri ya Kiislamu.