Pezeshkian: Nchi za Kiislamu zinapaswa kuzuia kuendelea jinai Gaza kupitia diplomasia amilifu
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza haja ya kufanyika juhudi za pamoja za nchi za Kiislamu ili kukomesha maafa ya binadamu huko Gaza.
Masoud Pezeshkian amesema hayo katika mazungumzo yake kwa njia ya simu na Anwar Ibrahim, Waziri Mkuu wa Malaysia.
Rais wa Iran amesema: "Maafa yanayofanywa na utawala wa Kizayuni huko Gaza hayakubaliki kwa mtu yeyote aliye huru, na ninatumai kuwa nchi za Kiislamu zitakomesha jinai hizo kupitia diplomasia amilifu na mashinikizo ya kidiplomasia, na zitakabiliana na hali hiyo kwa mshikamano, umoja na uwajibikaji.
Rais Pezeshkian amesisitiza kuwa: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima imekuwa ikitetea haki za wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina, na nchi nyingine za Kiislamu pia zinapaswa kuchukua misimamo thabiti na amilifu zaidi ya kuwatetea wananchi madhulumu wa Palestina na Gaza na kusema juhudi za pamoja za kukabiliana na jinai za utawala wa Kizayuni wa Gaza zitasaidia sana.
Katika mazungumzo hayo ya simu, Waziri Mkuu wa Malaysia amelaani pia jinai za Israel huko Gaza na kusema: "Serikali ya Kuala Lumpur imetoa tamko kali dhidi ya jinai za Israel huko Gaza na inaendeleza juhudi kubwa za kidiplomasia kukomesha mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina. "Tunatumai kuwa kwa ushirikiano na msaada wa nchi nyingine za Kiislamu, tunaweza kukomesha jinai hizo", amesema Anwar Ibrahim.