Iran yamnyonga jasusi mwingine wa shirika la Mossad
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i129236-iran_yamnyonga_jasusi_mwingine_wa_shirika_la_mossad
Iran jana Jumatano ilimnyonga mtu aliyepatikana na hatia ya kufanya ujasusi kwa maslahi ya Israel na kutoa taarifa kuhusu mwanasayansi wa nyuklia aliyeuawa katika mashambulizi ya Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu, mwezi Juni mwaka huu.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Aug 07, 2025 01:01 UTC
  • Iran yamnyonga jasusi mwingine wa shirika la Mossad

Iran jana Jumatano ilimnyonga mtu aliyepatikana na hatia ya kufanya ujasusi kwa maslahi ya Israel na kutoa taarifa kuhusu mwanasayansi wa nyuklia aliyeuawa katika mashambulizi ya Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu, mwezi Juni mwaka huu.

Roozbeh Vadi, aliyepatikana na hatia ya kufanya ujasusi na kushirikiana na Israel, alinyongwa Jumatano asubuhi baada ya mchakato wa kisheria na uthibitisho wa mwisho wa hukumu yake ya kifo katika Mahakama ya Juu.

Shirika la habari la mahakama la Mizan limeripoti kwamba, Roozbeh Vadi, alifanya kazi katika mojawapo ya "mashirika muhimu na nyeti" ya Iran, jambo ambalo lilimuwezesha kupata taarifa za siri ambazo alizivujisha baada ya kuajiriwa mtandaoni na shirika la ujasusi la kigeni la Israel, Mossad.

Ripoti ya shirika hilo imeeleza kuwa Vadi alifanya uhalifu wa aina mbalimbali dhidi ya usalama wa ndani na nje wa nchi, na kuvuruga pakubwa usalama wa umma.

Idadi ya majasusi walionyongwa kwa kupatikana na hatia ya kufanya ujasusi kwa maslahi ya Israel imeongezeka mwaka huu nchini Iran, na takriban hukumu nane za kifo zimetekelezwa katika miezi michache iliyopita.

Ripoti zinaonyesha kwamba, zaidi ya majasusi 700 waliokuwa wakishirikiana na Mossad wamekamatwa kote nchini Iran baada ya uvamizi wa Israel dhidi ya nchi hii mwezi Juni.

Israel ilianzisha mashambulizi ya anga dhidi ya Iran kwa muda wa siku 12 mwezi Juni mwaka, na Iran ilijibu kwa mashambulizi makali ya makombora na ndege zisizo na rubani yaliyoilazimisha Israel na Marekani kutangaza kuusitisha vita.