Rais wa Iran: Tunakaribisha ustawishaji mahusiano ya kujenga na nchi zote duniani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i129394-rais_wa_iran_tunakaribisha_ustawishaji_mahusiano_ya_kujenga_na_nchi_zote_duniani
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, taifa hili linakaribisha mahusiano na ushirikiano na mataifa yote ya dunia.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Aug 10, 2025 23:44 UTC
  • Rais Masoud Pezeshkian
    Rais Masoud Pezeshkian

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, taifa hili linakaribisha mahusiano na ushirikiano na mataifa yote ya dunia.

Rais Masoud Pezeshkian amesema hayo katika hafla ya kupokea hati za utambulisho za mabalozi wapya wa nchi tisa hapa nchini na kueleza kwamba, ni lazima tushirikiane, tuwe pamoja na kuimarishana katika njia ya kuendeleza amani, utulivu, utulivu na ustawi kwa wote.

Amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inakaribisha kuendelezwa kwa uhusiano wenye kujenga na ushirikiano na nchi zote duniani kwa msingi wa kuheshimiana.

Jana Jumapili, wakati wa hafla ya kupokea hati za utambulisho za mabalozi wapya wa Ethiopia, Estonia, Djibouti, Laos, Cambodia, Burundi, Latvia, Myanmar na Nepal, Masoud Pezeshkian alisema: "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inataka kupanua uhusiano wa kirafiki na ushirikiano wenye kujenga na nchi zote duniani."

Rais Pezeshkian amesema kuwa, Iran iko tayari na inapenda kupanua uhusiano na nchi hizo katika nyanja zote za kisiasa, kiuchumi, kibiashara, kiutamaduni, kisayansi na kiteknolojia, kwa kuzingatia kuheshimiana na ili kuhakikisha manufaa ya pande zote mbili.

Aidha katika hafla hiyo, Rais Pezeshhkian ameashiria kuendelea na kushadidi jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya wananchi wanaodhulumiwa na wasio na ulinzi wa Gaza na kusema: "Nchi zote duniani hususan nchi za Kiislamu zinapaswa kufanya juhudi kubwa zaidi na kushirikiana ili kukomesha jinai hizo, kuondoa mzingiro na kutoa misaada isiyo na kikomo na ya kina kwa watu wasio na hatia wa Gaza."