Kiongozi Muadhamu asisitiza utekelezaji wa makubaliano ya kimkakati ya Iran na China
Sambamba na safari ya Rais Masoud Pezeshkian wa Iran nchini China kwa ajili ya kushiriki katika Mkutano wa Shanghai, akaunti rasmi za Ofisi ya Kuhifadhi na Kuchapisha Kazi za Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei kwenye mitandao ya kijamii imechapisha baadhi ya matamshi ya Imam Khamenei kuhusu umuhimu wa uhusiano wa Iran na China kwa lugha ya Kichina.
Akaunti za Ofisi ya Kuhifadhi na Kuchapisha Kazi za Kiongozi Muadhamu katika mitandao ya kijamii imeichapisha taarifa za Kiongozi Muadhamu kuhusu uwezo wa Iran na China katika jukwaa la kimataifa na haja ya kutekelezwa makubaliano ya kimkakati kati ya nchi hizo mbili.
Sehemu moja ya ujumbe huo wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: "Iran na China, zikiwa na historia ya kale ya ustaarabu katika pande zote mbili za Asia, zina uwezo wa kufanya mabadiliko katika nyanja ya kieneo na kimataifa. Utekelezaji wa vipengele vyote vya makubaliano ya kistratijia ndio ufunguo wa njia hiyo."
Jana Jumapili, kabla ya kuelekea China kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa 25 wa Baraza la Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai (SCO) na ule wa SCO+, Rais Masoud Pezeshkian wa Iran alisema kuwa mkutano ujao wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai (SCO) unatoa fursa ya kukabiliana na hatua za kujichuulikia maamuzi ya upande mmoja za Marekani na Ulaya katika masuala ya kimataifa.
Pezeshkian amesisitiza kuwa: Mkutano wa 25 wa Baraza la Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai (SCO) unawapa washiriki fursa nzuri na muhimu ya kukurubisha mitazamo yao katika nyanja za kisayansi, kiutamaduni, kiuchumi, kisiasa na kiusalama na kuimarisha ushirikiano kati yao.
Akizungumzia umuhimu wa mkutano huo, Rais Pezeshkian aliongeza kuwa, nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai zinawakilisha karibu watu bilioni 2.5, na zinachangia zaidi ya asilimia 40 ya uchumi wa dunia.