Kwa nini njama zote za Marekani dhidi ya Iran daima zinafeli?
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i135522-kwa_nini_njama_zote_za_marekani_dhidi_ya_iran_daima_zinafeli
Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema kwamba, watu wa Iran wataendelea kusimama imara kulinda na kutetea nchi yao, akisisitiza kuwa, njama yoyote ya Marekani dhidi ya Iran itashindwa tu kama zilivyoshindwa njama zao zote za huko nyuma.
(last modified 2026-01-16T02:10:36+00:00 )
Jan 16, 2026 02:10 UTC
  • Amir-Saeid Iravani
    Amir-Saeid Iravani

Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema kwamba, watu wa Iran wataendelea kusimama imara kulinda na kutetea nchi yao, akisisitiza kuwa, njama yoyote ya Marekani dhidi ya Iran itashindwa tu kama zilivyoshindwa njama zao zote za huko nyuma.

Amir-Saeid Iravani, Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesisitiza katika barua yake kwa Baraza la Usalama kwamba "Marekani na utawala wa Kizayuni zinahusika na kupoteza maisha raia hasa vijana, katika matukio ya hivi karibuni nchini Iran."

Katika barua hiyo, ambayo nakala yake ametumiwa pia Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Iravani amesema kuwa, Washington inatumia vikwazo, vitisho na kuchochea machafuko ili kutafuta kisingizio cha kuingia kijeshi nchini Iran.

Mwakilishi wa kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amelitaka Baraza la Usalama na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kulaani jinai na uchokozi wa Marekani na kuingilia kwake masuala ya ndani ya Iran kama ambavyo amewataka pia walaani vitisho vya Trump vya kutumia nguvu dhidi ya Tehran akisisitiza kuwa: Umoja wa Mataifa unapaswa kuionya Marekani isijaribu kufanya kosa lolote la kimahesabu linaloweza kuifanya ianzishe vita vingine dhidi ya Iran.

Katika kuelezea kushindwa njama za Marekani dhidi ya Iran katika miaka ya hivi karibuni amesema kuwa, sababu kuu ya matatizo ya eneo hili la Asia Magharibi na kukosekana amani na utulivu katika eneo hili, ni uingiliaji wa madola ajinabi katika masuala ya ndani ya eneo hili.

Inachopigania Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kuwa huru na kutoingiliwa mambo yake ya ndani na hicho ni kitu ambacho kila nchi inakipigania. Iran inataka mataifa ya eneo hili yashirikiane na kutatua yenyewe masuala yao kwa kushirikiana na kushauriana baina yao na kutoruhusu madola ajinabi kuingilia masuala ya eneo lao. Iran muda wote imesimama kidete kuwatetea wanyonge na kupigania haki na yote hayo yanakinzana na njama za Marekani ambayo inajaribu kudhibiti kila kitu kwa manufaa yake binafsi na kwa madhara ya mataifa ya eneo hili.

Mamilioni kwa mamilioni ya wananchi wa Iran katika kuunga mkono Jamhuri ya Kiislamu

Hali ya kijiografia ya Iran pia ina nafasi muhimu sana katika kupunguza nguvu za Marekani kwenye eneo hili. Iran iko kwenye makutano ya Asia Magharibi, Asia ya Kati, Caucasus, Bara Hindi na bahari kubwa na muhimu sana duniani. Iran ina ushawishi mkubwa pia katika matukio ya kikanda na hiyo ni moja ya sababu kuu za kushindwa sera za Marekani na ndio maana Washington haiwezi kupuuza ukweli huu.

Viongozi wa Iran wamekuwa wakisisitiza mara kwa mara kwamba njama za Marekani dhidi ya Iran hazikufanikiwa katika miaka iliyopita na kamwe hazitofanikiwa kabisa katika siku zijazo. Uwezo wa ulinzi na Muqawama wa Iran umevuruga njama za Marekani na unaendelea kuzivuruga kwa miaka mingi sasa na hiyo ndiyo sababu ya uadui mkubwa wa dola la kiistikbari la Marekani dhidi ya Iran ya Kiislamu.

Katika upande wa kimataifa pia, taasisi, jumuiya na miungano ya kisiasa na kiuchumi ya nchi huru, ikiwa ni pamoja na kundi la BRICS na Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai, zimeleta mabadiliko ya kimuundo katika mfumo wa kimataifa na hivi sasa ndoto za Marekani za kutaka kuwa dola pekee lenye nguvu duniani na linaloamua mambo yote, zimezimwa.

Baada ya kuanza machafuko nchini Iran katika siku za hivi karibuni, Marekani na serikali za nchi za Magharibi zilijaribu kutumia kisiasa matukio hayo kwa kurudia tabia zao zilezile za kusambaza habari za uongo na kutia chumvi kupindukia matukio ya Iran. Maafisa wa Marekani na wa madola ya Magharibi wanatangaza waziwazi kuwaunga mkono magaidi na magenge ya mamluki ambao wamefanya jinai na ukatili mkubwa dhidi ya wananchi wa Iran na mali zao. 

Lakini Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa mara nyingine tena imefanikiwa kuzima njama ovu za Marekani-Magharibi na Uzayuni kwa kutegemea uungaji mkubwa mkubwa wa wananchi wake ambao Jumatatu ya tarehe 12 Januari 2026 walijitokeza mitaani kwa makumi ya mamilioni, kuiunga mkono Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kona zote wa nchi. Huo ni ushahidi mwingine wa kufeli mahesabu ya madola ya kibeberu hasa Marekani kuhusu Iran.

Matukio ya hivi karibuni ya nchini Iran yameonesha kuwa kitendo cha Marekani cha kuingilia moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja masuala ya ndani ya Iran kimekuwa na athari tofauti na wanavyotarajia maadui, kwani muda wote hatua kama hizo huwa zinaongeza mshikamano wa wananchi wa Iran na utiifu wao kwa Jamhuri ya Kiislamu.