Tehran yahimiza marekebisho 'makubwa' katika mbinu 'zisizojenga' za EU
-
Araqchi na Kombos
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi, amesema Umoja wa Ulaya unahitajika kufanya marekebisho makubwa katika mbinu zake "zisizo za kujenga" kuhusu Tehran.
Araqchi alitoa kauli hiyo katika mazungumzo ya simu, jana Ijumaa, na Waziri wa Mambo ya Nje wa Cyprus, Constantinos Kombos, ambaye nchi yake inashikilia urais wa Umoja wa Ulaya (EU) kwa zamu.
Araqchi amekosoa mbinu zisizofaa za EU kuhusu Iran, hasa hatua ya hivi karibuni ya kihasa ya Baraza la Umoja wa Ulaya ya kuorodhesha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) kuwa "shirika la kigaidi" na kuingilia kati bila sababu masuala ya ndani ya Iran.
Mnamo Januari 30, Umoja wa Ulaya uliiweka IRGC kwenye orodha yake eti ya makundi ya kigaidi kwa sababu ya kile ilichodai ni ukandamizaji wa Iran dhidi ya waandamanaji waliosababisha vurugu kote nchini kwa uchochezi na ufadhili wa viongozi wa Marekani na Israel, mwishoni mwa Desemba.
Mamlaka za Iran zimethibitisha kwamba mashirika ya ujasusi ya Marekani na Israel yalihusika moja kwa moja katika machafuko hayo, yakitoa ufadhili, mafunzo na misaada ya vyombo vya habari kwa waandamanaji na magaidi wenye silaha waliofanya machafuko mitaani.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran pia amemwambia mwenzake wa Cyprus kwamba misimamo isiyo sahihi ya Umoja wa Ulaya kuhusu matukio ya kikanda, ikiwa ni pamoja na mauaji ya kimbari yanayofanywa na Israel huko Gaza na uhalifu wa utawala huo dhidi ya nchi za kikanda, ni ukiukaji wa kanuni ya utawala wa sheria na kuheshimu kanuni za sheria za kimataifa.
Kwa upande wake, Constantinos Kombos amekaribisha kuanza duru mpya ya mazungumzo ya nyuklia kati ya Iran na Marekani, akizungumzia umuhimu wa kuendelezwa mazungumzo hayo na kupunguza mvutano.