IRGC: Tumewavurumishia maadui makombora 700, droni 3,600 mpaka sasa
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i137410-irgc_tumewavurumishia_maadui_makombora_700_droni_3_600_mpaka_sasa
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran (IRGC) limesema limepiga shabaha za Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel kwa makombora zaidi ya 700 na ndege zisizo na rubani 3,600 tangu Jamhuri ya Kiislamu ianzishe operesheni za kulipiza kisasi cha mashambulizi ya kichokozi ya maadui hao mwishoni mwa Februari mwaka huu.
(last modified 2026-03-17T03:38:40+00:00 )
Mar 17, 2026 03:38 UTC
  • IRGC: Tumewavurumishia maadui makombora 700, droni 3,600 mpaka sasa

Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran (IRGC) limesema limepiga shabaha za Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel kwa makombora zaidi ya 700 na ndege zisizo na rubani 3,600 tangu Jamhuri ya Kiislamu ianzishe operesheni za kulipiza kisasi cha mashambulizi ya kichokozi ya maadui hao mwishoni mwa Februari mwaka huu.

Taarifa ya IRGC haijatoa maelezo kuhusu wakati wa kufanyika mashambulizi hayo ya kisasi, maeneo yaliyopigwa au ukubwa wa uharibifu uliosababisha kwenye operesheni zake hizo za makombora na droni.

Hata hivyo IRGC imesema imeshambulia kwa makombora na droni kambi za kijeshi, viwanda pamoja na maeneo ya mikusanyiko ya wanajeshi wa Marekani katika maeneo tofauti ya eneo hili la Asia Magharibi.

SEPAH imesema imetumia makombora mazito aina ya Khorramshahr yenye kichwa chenye uzito wa tani mbili, pamoja na makombora Kheibar‑Shekan, Qadr, Emad, na kwa mara ya kwanza katika Operesheni Ahadi ya Kweli 4, kombora la kimkakati la Sejjil limetumika.

Kwa mujibu wa picha za satalaiti, Vikosi vya Ulinzi vya Iran vimefanikiwa kusambaratisha asilimia 80 ya vituo vya rada na maeneo mengine ya kistratejia ya jeshi la Marekani katika eneo.

Siku ya Jumatatu, Idara ya Mawasiliano ya Umma ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran (IRGC) ilitangaza kuwa jeshi hilo limetekeleza wimbi la 56 la mashambulizi ya makombora, kama sehemu ya Operesheni ya Ahadi ya Kweli 4.

Katika operesheni hiyo, shabaha zilizolengwa ni pamoja na Kamandi ya Lojistiki ya eneo la kusini na bohari la kuhifadhia makombora ya Rafael katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu (Israel), na vile vile kambi ya kijeshi ya Marekani ya Dar Adid.