Jeshi la Iran limelenga Uwanja wa Ndege wa Ben‑Gurion kwa droni
-
Droni za Arash-2
Msemaji wa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa jeshi hilo limetekeleza shambulio kwa mafanikio dhidi ya Uwanja wa Ndege wa Ben‑Gurion katika mji wa Lod umbali wa kilomita 15 kusini mashariki mwa Tel Aviv, kwa kutumia droni ya kisasa ya Arash‑2.
Brigedia Mohakmmad Akarminiyaa, akitoa maelezo kuhusu operesheni ya hivi karibuni dhidi ya uwanja wa ndege wa Ben‑Gurion wa utawala ghasibu wa Israel, amesema kuwa sehemu kubwa ya droni zilizotumika zilikuwa aina ya Arash‑2 zenye masafa ya kilomita 2000, ambazo kutokana na uwezo wa kukwepa rada, ziliweza kulenga shabaha kwa urahisi.
Brigedia Akarminiyaa, amongeza kuwa: “Droni nyingi tulizotumia dhidi ya Uwanja wa Ben‑Gurion ni Arash‑2, ambayo ni toleo lililoendelezwa zaidi na lenye nguvu kuliko Kian na Arash‑1. Ina uwezo wa kufika umbali wa kilomita 2000 na katika istilahi yetu huitwa droni zinazolenga maeneo ya Israel.”
Msemaji wa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa droni hizi hupenya kwa urahisi kwenye mifumo ya ulinzi wa anga na kuwa vigumu kwa upande wa pili kuzigundua.
Brigedia Akarminiyaa amesisitiza kuwa droni hizi zina uwezo wa kulenga kwa usahihi mkubwa, na kuongeza: “Arash‑2 hutengenezwa kwa kasi kubwa na maandalizi yake ya kurushwa ni ya haraka sana. Kwa hivyo, tunapofanya uamuzi, tunaweza kuzindua idadi kubwa kwa urahisi.”
Msemaji wa jeshi, akizungumzia shambulio dhidi ya Uwanja wa Ben‑Gurion, amesema: “Uwanja huu ni mkubwa zaidi kijeshi kwa utawala wa Kizayuni wa Israel . Katika mzozo huu, umekuwa mahali pa kukusanya ndege za mafuta ambazo zinatumika kujaza mafuta ndege za kivita zinazoruka angani katika mashambulizi dhidi ya Iran. Aidha amesema karibu na uwanja huu kuna viwanda vya matengenezo ya ndege, jambo linaloupa umuhimu wa kijeshi katika utawala ghasibu wa Israel.
Msemaji wa Jeshi la Iran amebainisha umuhimu wa kiuchumi wa uwanja huo kwa utawala wa Kizayuni, na kusema: :Kwa kuwa shughuli kubwa za biashara hupitia uwanja wa Ben‑Gurion, uwanja huu ni kama mshipa mkuu wa uchumi wa utawala wa Kizayuni.”
Akizungumzia malengo ya operesheni hiyo amesema: “Katika mashambulizi dhidi ya Uwanja wa Ben‑Gurion, tulilenga ndege za kijeshi, matanki ya mafuta, miundombinu ya rada na miundombinu ya uwanja wa ndege. Taarifa tulizonazo zinaonyesha kuwa safari za ndege zimepata hitilafu.”