Iran: Dunia imechoshwa na hadithi za uongo za Marekani na Israel
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, ameashiria msimamo wa Katibu Mkuu wa Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi-NATO- kuhusu kukataa madai ya hivi karibuni ya maafisa wa utawala wa Kizayuni Israel kuhusu tishio la makombora ya Iran kwa Ulaya na kuandika katika mtandao wa X kuwa dunia imechoka na simulizi za uongo za Marekani na Israel.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la ISNA, Ismail Baqaee , msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran , ameandika kuwa: “Hata pale mtu kama Katibu Mkuu wa NATO , ambaye amejipatia sifa mbaya kwa kushinikiza wanachama wa NATO kuunga mkono vita visivyo halali vya Marekani na Israel dhidi ya Iran , anapokataa kuthibitisha uongo wa hivi karibuni wa Waisraeli, jambo hili ni lenye uzito mkubwa. Dunia imechoshwa na simulizi zinazoegemea mbinu za upotoshaji.”
Katika siku mbili zilizopita, baadhi ya maafisa wa Israel walinukuliwa na vyombo vya habari vya Marekani wakidai kuwa Iran ilirusha makombora kuelekea kituo cha kijeshi cha Uingereza huko Diego Garcia, na wakajaribu kuwasilisha mpango wa makombora wa Iran kama tishio kwa Ulaya. Hata hivyo, Katibu Mkuu wa NATO ameyakana waziwazi madai hayo ya maafisa wa utawala wa Kizayuni.
Kituo cha kijeshi cha Diego Garcia kikao katika Bahari ya Hindi umbali wa zaidi ya kilomita 4000 kutoka Iran. Baadhi ya ndege za kivita za Marekani ziko katika kituo hicho.
Iran imekuwa ikisisitiza kuwa masafa ya makombora yake ni kilomita 2000 kwa lengo la kukabiliana na utawala wa Kizayuni wa Israel.