Marais wa Iran na Ufaransa wazungumza kuhusu kupunguza mvutano Asia Magharibi
Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, amesema kuwa katika mazungumzo ya simu na Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, walijadili suala la Lango Bahari la Hormuz na namna ya kupunguza mvutano katika eneo la Asia Magharibi (Mashariki ya Kati).
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la IRIB, Macron aliandika Jumanne usiku katika ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa X kwamba katika mazungumzo hayo walizungumzia “kulinda miundombinu ya nishati na ya kiraia” pamoja na “uhuru wa usafiri wa baharini katika Lango Bahari la Hormuz”.
Ameongeza kuwa ameihimiza Iran kushiriki kwa nia njema katika mazungumzo yanayolenga kusawazisha njia ya kupunguza mvutano na kuweka mfumo wa kushughulikia matarajio ya jumuiya ya kimataifa kuhusu programu ya nyuklia, makombora ya balistiki, na pia shughuli za kikanda za Iran.
Katika mazungumzo hayo ya simu Rais Pezeshkian alimwambia Macron kwamba chanzo cha ukosefu wa usalama na kutokuwepo kwa uthabiti katika eneo ni vitendo vya uhasama vya utawala wa Kizayuni, pamoja na mauaji yaliyofanyika Gaza na Lebanon, na pia kuanzishwa kwa vita viwili vilivyolazimishwa dhidi ya Iran kwa ushirikiano wa Marekani na utawala wa Israel. Aidha, amekosoa mtazamo wa baadhi ya nchi za Ulaya ambao unaunga mkono uhalifu wa utawala huo na wa Marekani katika eneo la Asia Magharibi, huku akizitaka ziheshimu sheria za kimataifa na utawala wa sheria duniani.
Shambulio la pamoja la kijeshi la Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran lilianza asubuhi ya tarehe 28 Februari 2026 sawa na tarehe 10 ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Hatua hiyo ilifanyika wakati ambapo mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani, kwa upatanishi wa baadhi ya nchi za eneo, yalikuwa yanaendelea.
Kufuatia kuanza kwa hujuma hiyo kijeshi na kigaidi ambayo ingali inaendelea, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikitekeleza operesheni za kulipiza kisasi kwa kutumia makombora na ndege za kivita zisizo na rubani.
Majeshi ya Iran yanaendelea kutekeleza mashambulizi dhidi ya ngome za kijeshi na kiuchumi za utawala wa kizayuni wa Israel na pia dhidi ya vituo na kambi za majeshi ya kigaidi ya Marekani katika nchi za eneo la Asia Magharibi.