Iran yakataa pendekezo la Marekani, yaweka masharti matano ya kukomesha vita
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i137592-iran_yakataa_pendekezo_la_marekani_yaweka_masharti_matano_ya_kukomesha_vita
Iran imetoa majibu hasi kwa pendekezo la Marekani linalolenga kukomesha vita vinavyoendelea hivi sasa, ikisisitiza kwamba jambo hilo litatokea kwa masharti na ratiba ya Tehran, afisa mkuu wa usalama na kisiasa ameambia Press TV.
(last modified 2026-04-19T09:26:01+00:00 )
Mar 26, 2026 04:52 UTC
  • Tehran, Iran
    Tehran, Iran

Iran imetoa majibu hasi kwa pendekezo la Marekani linalolenga kukomesha vita vinavyoendelea hivi sasa, ikisisitiza kwamba jambo hilo litatokea kwa masharti na ratiba ya Tehran, afisa mkuu wa usalama na kisiasa ameambia Press TV.

Akizungumza na Press TV, afisa huyo amesema Iran haitamruhusu Rais wa Marekani, Donald Trump, kuamua muda wa mwisho wa vita hivyo.

"Iran itamaliza vita itakapoamua kufanya hivyo na wakati masharti yake yatakapotimizwa," afisa huyo amesema, akisisitiza azma ya Tehran ya kuendelea kujilinda na kutoa vipigo vizito dhidi ya adui hadi matakwa yake yatakapotimizwa.

Kwa mujibu wa afisa huyo, Washington imekuwa ikiomba kufanya mazungumzo kupitia njia mbalimbali za kidiplomasia, ikitoa mapendekezo ambayo Tehran inayaona kama "ya kupita kiasi" na yasiyo na uhusiano wowote na hali halisi ya kushindwa Marekani kwenye uwanja wa vita.

Afisa huyo amefananisha raundi mbili za awali za mazungumzo yaliyofanyika baina ya Iran na Marekani katika majira ya machipuo na ya baridi kali ya 2025, akizitaja kama za udanganyifu.

Katika hali zote mbili, afisa huyo amesisitiza, Marekani haikuwa na nia ya dhati ya kushiriki katika mazungumzo yenye maana, na baadaye ilifanya mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Iran.

Kwa kuzingatia ukweli huo, Tehran imeainisha ombi la hivi karibuni la Marekani, ambalo limetolewa kupitia mpatanishi rafiki wa kikanda, kama njama ya kuzidisha mvutano na imetoa majibu hasi kwa ombi hilo.

Afisa huyo ameeleza masharti matano mahususi ambayo Iran itayakubali kwa ajili ya kukomesha vita, ambayo ni:

-Kukomesha kabisa "uchokozi na mauaji" ya kigaidi yanayofanywa na adui hapa nchini.

- Kuanzishwa mifumo thabiti ya kuhakikisha kwamba vita havirudiwi tena dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.

- Kutolewa dhamana ya fidia na uharibifu wa vita na fidia nyingine zilizoelezwa kwa uwazi.

- Kukomeshwa vita katika pande zote na kwa makundi yote husika ya muqawama katika eneo lote la Asia Magharibi.

- Na Utekelezaji wa mamlaka ya Iran katika Lango-Bahari la Hormuz ambayo yatabaki kuwa haki ya asili na kisheria ya Iran, na ni dhamana ya utekelezaji wa majukumu ya upande mwingine, na ulazima kutambuliwa rasmi.

Afisa huyo ameeleza kwamba masharti haya ni pamoja na matakwa yaliyowasilishwa hapo awali na Tehran wakati wa duru ya pili ya mazungumzo huko Geneva, ambayo yalifanyika siku chache tu kabla ya Marekani na Israel kuanzisha uchokozi mpya dhidi ya Iran mnamo Februari 28.

Iran imewafahamisha wapatanishi wote wanaotenda kwa nia njema kwamba kusitisha mapigano kunategemea kukubalika kwa masharti yake yote.

"Hakuna mazungumzo yatakayofanyika kabla ya hapo," afisa huyo amesisitiza, na kusema Iran itaendeleza operesheni za kujilinda hadi masharti yaliyoainishwa yatakapotimizwa.

"Vita hivi vitafikia tamati wakati Iran itakapoamua kuvimaliza, si wakati Trump atakapofikiria kumalizika kwake," ameongeza afisa huyo wa Iran.