Pezeshkian: Nchi za Kiislamu zisiwaruhusu maadui kupanda mbegu za mifarakano
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i137606-pezeshkian_nchi_za_kiislamu_zisiwaruhusu_maadui_kupanda_mbegu_za_mifarakano
Rais wa Iran amesema katika mazungumzo ya simu na Waziri Mkuu wa Malaysia kwamba nchi za Kiislamu hazipaswi kuwaruhusu maadui kupanda mbegu za mifarakano na kuwasha moto wa vita.
(last modified 2026-03-26T23:05:54+00:00 )
Mar 26, 2026 23:05 UTC
  • Rais Masoud Pezeshkian  wa Iran (kulia) na Waziri Mkuu wa Malaysia Anwar Ibrahim
    Rais Masoud Pezeshkian wa Iran (kulia) na Waziri Mkuu wa Malaysia Anwar Ibrahim

Rais wa Iran amesema katika mazungumzo ya simu na Waziri Mkuu wa Malaysia kwamba nchi za Kiislamu hazipaswi kuwaruhusu maadui kupanda mbegu za mifarakano na kuwasha moto wa vita.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la IRIB, Rais Masoud Pezeshkian  wa Iran amezungumza kwa simu na Waziri Mkuu wa Malaysia Anwar Ibrahim kuhusu matukio ya kikanda na kimataifa yaliyofuatia shambulio la Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Iran.

Katika mazungumzo hayo, Rais Pezeshkian ametoa  shukrani kwa msimamo wa kimsingi na wenye thamani wa serikali na wananchi wa Malaysia kwa kulaani vita vya Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran.

Rais Pezeshkian amesema hatua ya Iran ya kulenga vituo na kambi za kijeshi za Marekani zilizo katika baadhi ya nchi za eneo ni jibu linalotarajiwa kwa chanzo cha mashambulizi yaliyofanywa dhidi ya Iran. Amesisitiza kwamba nchi za Kiislamu hazipaswi kuwaruhusu maadui kutumia suala hili kupanda mifarakano na kuchochea moto wa vita katika eneo hilo.

Rais Pezeshkian amesisitiza kuwa Iran haijawahi kufuatilia umiliki wa silaha za nyuklia, na kwamba ripoti nyingi za Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) zimethibitisha ukweli huo. Amesema madai kwamba Iran inajaribu kupata silaha za atomiki ni kisingizio kinachotumiwa kuhalalisha mashambulizi dhidi ya taifa la Iran.

Ameongeza kuwa: “Tunataka vita vikome kabisa na kuwepo kwa usalama na utulivu katika eneo hili, na tunatumaini kwa msaada wa nchi ndugu za Kiislamu tutaweza kulinusuru eneo letu dhidi ya janga ambalo maadui wanajaribu kulisababisha.”

Katika mazungumzo hayo ya simu, Waziri Mkuu wa Malaysia pia alitoa salamu za rambirambi kufuatia kuuawa shahidi kwa Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu pamoja na baadhi ya makamanda, viongozi na raia wa Iran katika mashambulizi ya Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran. Amebainisha mshikamano wake na serikali na wananchi wa Iran wakati huu wa majonzi.

Anwar Ibrahim pia ameashiria kupitishwa kwa azimio katika Bunge la Malaysia—kwa pendekezo la waziri mkuu—linalolaani vita vya Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Iran, na kusisitiza msimamo wa kimsingi wa nchi yake wa kupinga na kulaani aina yoyote ya uvamizi dhidi ya mamlaka ya kitaifa na mipaka ya Iran.

Waziri Mkuu wa Malaysia, akithibitisha msimamo ambao aliuita wa haki kuhusu ulazima wa kumaliza vita dhidi ya Umma wa Kiislamu katika eneo lote, na kuhakikisha kuwa mashambulizi dhidi ya Iran hayatajirudia. Aidha amebainisha wasiwasi wake kuhusu kuongezeka kwa mvutano katika eneo la Asia ya Magharibi. Amesisitiza umuhimu wa juhudi za kisiasa za nchi za Kiislamu ili kuimarisha utulivu na usalama katika eneo hilo.