Iran yatafakari kujiondoa mkataba wa nyuklia wa NPT
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i137652-iran_yatafakari_kujiondoa_mkataba_wa_nyuklia_wa_npt
Ripoti zinaonyesha kuwa suala la kujiondoa katika Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa Silaha za Nyuklia (NPT) sasa limewekwa katika ajenda ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
(last modified 2026-03-29T01:06:41+00:00 )
Mar 29, 2026 01:06 UTC
  • Iran yatafakari kujiondoa mkataba wa nyuklia wa  NPT

Ripoti zinaonyesha kuwa suala la kujiondoa katika Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa Silaha za Nyuklia (NPT) sasa limewekwa katika ajenda ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Tasnim, taasisi kadhaa husika nchini Iran, zikiwemo Bunge, zinapitia kwa dharura suala la kujiondoa katika NPT. Inaripotiwa kuwa mtazamo unaozidi kuimarika ndani ya Iran ni kwamba hakuna tena haja ya kuendelea kubaki katika mkataba huo.

Kwa mujibu wa NPT, Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) linapaswa kuweka mazingira ya kulinda na kusaidia  Iran kupata teknolojia ya nyuklia ya matumizi ya amani pamoja na vifaa vyake. Hata hivyo, wakati Mkurugenzi Mkuu wa IAEA, Rafael Grossi, anatoa kauli zinazotafsiriwa kama kuhimiza adui kutekeleza mashambulizi dhidi ya vituo vya  nyuklia vya Iran, na adui wa Marekani na Israel anaposhambulia miundombinu ya Iran bila kizuizi au hata kulaaniwa na IAEA, basi hakuna tena sababu ya Iran kubaki ndani ya NPT.

Kujiondoa katika NPT hakumaanishi kuelekea katika utengenezaji wa silaha za nyuklia; bali kunakusudia kuzuia kuendelea kwa shughuli za ujasusi za Marekani na utawala wa Israel zinazofanyika chini ya kivuli cha wakaguzi wa IAEA.

Mkataba wa NPT kimsingi ulianzishwa kwa lengo la kusaidia nchi mbalimbali kuzalisha na kutumia nishati ya nyuklia kwa madhumuni ya amani. Hata hivyo, licha ya ukweli kwamba utawala wa Kizayuni wa Israel, ambao unamiliki silaha hatari za nyuklia, haujawahi kuwa mwanachama wa mkataba huo na haujawahi kukabiliwa na shinikizo kujiunga nao, Iran imeendelea kuwa mwanachama wa NPT.

Mbali na NPT, ambayo kimsingi ni mfumo wa udhibiti na, kwa dhahiri, wa kusaidia katika sekta ya nyuklia, Iran pia imekubali Itifaki ya Ziada katika makubaliano mbalimbali, ikiwemo katika mapatano ya nyuklia ya  Mpango wa Pamoja wa Hatua Kamili (JCPOA), na hata imekwenda zaidi ya masharti ya Itifaki hiyo ya Ziada ili kuonyesha uwazi wake na utayari wa kushirikiana na mifumo ya uangalizi.

Hata hivyo, uanachama wa Iran katika NPT haujaleta manufaa yoyote kwa nchi hiyo katika kupata teknolojia ya nyuklia kwa matumizi ya amani. Kinyume chake, mkataba huo wa NPT umekuwa ukisaidia shughuli za ujasusi za Israel na Marekani dhidi ya Iran. Maadui hao wamefanya mara kadhaa hujuma dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran kwa kutumia taarifa zinazotokana na Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA), na hata kufikia hatua ya kuvishambulia kwa mabomu. Katika vita vya sasa, Marekani na Israel zimedondosha mabomu katika vituo kadhaa vya nyuklia vya Iran bila kulaaniwa na IAEA.