Iran yakanusha kuwepo mazungumzo yoyote na Marekani
-
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baqaei
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baqaei, amesisitiza kuwa Tehran haijafanya mazungumzo ya moja kwa moja na Marekani, na amekanusha madai kwamba Jamhuri ya Kiislamu imekubali mapendekezo ya Washington, akieleza kauli hizo kuwa hazina msingi wowote.
Akizungumza katika mkutano wake wa kawaida na waandishi wa habari, Baqaei amekanusha madai ya Rais wa Marekani, Donald Trump kwamba Iran imekubali mapendekezo ya Marekani. Amesisitiza kuwa msimamo wa Iran umekuwa thabiti tangu mwanzo, ukipinga matakwa yaliyopitiliza na yasiyo ya busara ambayo yamewasilishwa kupitia wapatanishi.
Baqaei amesema kuwa hadi sasa Iran haijafanya mazungumzo ya moja kwa moja na Marekani.
Amefafanua kwamba kilichokuwepo ni ujumbe uliowasilishwa Tehran kupitia nchi au wahusika wa kati, unaoonyesha nia ya Marekani ya kutaka kufanya mazungumzo n Iran. Hata hivyo ameonya kuwa kila mara Marekani inapozungumzia diplomasia, jambo hilo linapaswa kuchunguzwa kwa tahadhari.
Ameongeza kuwa haijulikani ni kwa kiwango gani baadhi ya viongozi wa Marekani wenyewe wanaamini kauli zao kuhusu diplomasia. Baqaei amesisitiza kwamba msimamo wa Iran uko wazi na thabiti, na hauyumbi kama inavyobadilika mara kwa mara msimamo wa Marekani.
Amesema Iran daima inafahamu mfumo na misingi ya mazungumzo inayoyataka, akieleza kwamba mapendekezo yaliyowasilishwa kupitia njia za kati yalikuwa ya kupita kiasi na yasiyokubalika.
Akizungumzia mikutano iliyofanyika Pakistan, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema mikutano hiyo imefanyika katika mfumo uliowekwa na Pakistan yenyewe, na Iran haikuwa mshiriki wake.
Amebainisha kuwa ni jambo jema kuona nchi za kanda zikijali sala la kumalizika vita, lakini amesisitiza kuwa lazima itambulike ni nani aliyeanzisha uchokozi. Ameongeza kuwa haiwezi kutarajiwa Iran pekee ndiyo ijizuie, akisisitiza kwamba Iran ndiyo iliyoshambuliwa na siyo iliyoanzisha mapigano.
Akijibu madai ya Trump kwamba Iran imekubali mapendekezo ya Marekani, Baqaei alisema maafisa wa Marekani wanaweza kusema chochote wanachotaka, lakini ukweli ni kwamba hakuna mazungumzo yaliyofanyika kati ya Iran na Marekani.
Amesisitiza kuwa mawasiliano pekee yaliyokuwepo ni maombi ya Marekani ya kutaka mazungumzo yaliyowasilishwa kupitia nchi za tatu.
Baqaei ameongeza kuwa msimamo wa Iran uko wazi: kadiri uchokozi unavyoendelea, juhudi za Iran zitaendelea kujikita katika kujilinda.
Amemalizia kwa kusema kuwa madai kama hayo kutoka Marekani si ya kuaminika, akiongeza kuwa Iran imewahi kushuhudia moja kwa moja kuvunjwa kukiukwa kuli na usaliti katika mazungumzo yaliyopita.
Ikumbukwe kuwa mwezi Juni mwaka jana na mwezi Februari mwaka huu Marekani ikishirikiana na Israel ilianzisha vita dhidi ya Iran katikati ya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja.