Araghchi: Iran haijatoa jibu lolote kwa mapendekezo 15 ya Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i137710-araghchi_iran_haijatoa_jibu_lolote_kwa_mapendekezo_15_ya_marekani
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema: Tehran hadi sasa haijatoa jibu kwa mapendekezo 15 ya Marekani, wala haijawasilisha sharti lolote.
(last modified 2026-04-01T06:51:37+00:00 )
Apr 01, 2026 03:07 UTC
  • Sayyid Abbas Araghchi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran
    Sayyid Abbas Araghchi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema: Tehran hadi sasa haijatoa jibu kwa mapendekezo 15 ya Marekani, wala haijawasilisha sharti lolote.

Katika mahojiano yake na televisheni ya Al‑Jazeera ya Qatar, Sayyid Abbas Araghchi ametoa ufafanuzi kuhusu hali ya sasa ya ubadilishanaji wa ujumbe na Marekani, masharti ya Iran ya kumaliza vita, na pia kuhusu hali ya Lango Bahari la Hormuz.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kinachoendelea “si mazungumzo” bali ni kubadilishana ujumbe; ambao huwasilishwa moja kwa moja au kupitia “marafiki wa kikanda.”

Amesisitiza kuwa bado anapokea ujumbe kutoka kwa Steve Witkoff, mjumbe maalumu wa Marekani, lakini jambo hilo halimaanishi kuwa kuna mazungumzo yayonaendelea baina ya nch mbili.

Waziri Araghchi ameongeza kuwa ujumbe unaobadilishwa kwa kawaida huwa ni “tahadhari au mitazamo ya pande mbili” inayowasilishwa kupitia njia mbalimbali za kieneo.

Araghchi amesema hakuna mazungumzo yanayoendelea baina ya Iran na upande wowote kwa sura rasmi, na kwamba ujumbe hupitia Wizara ya Mambo ya Nje kwa uratibu kamili na taasisi za kiusalama.

Amesema pia kuwa ubadilishanaji wa jumbe unafanyika katika mfumo rasmi chini ya usimamizi wa Serikali na Baraza Kuu la Usalama wa Taifa.

Araghchi amesisitiza kuwa Iran haijatoa jibu kwa mapendekezo 15 ya Marekani kuhusu usitishaji vita, na pia haijawasilisha pendekezo au sharti lolote upande wake.

Amesema Tehran bado haijafanya uamuzi kuhusu asili ya mazungumzo yenyewe, na kwamba masharti ya Iran ya kumaliza vita “yapo wazi kabisa.”

Araghchi amesisitiza tena kuwa Iran “haitakubali kusitisha vita” bila kukomeshwa kabisa “vita kote katika kanda hii.”

Masharti aliyoyataja ni “dhamana ya kutokurudiwa kwa mashambulizi” na “kulipwa fidia ya hasara.”

Araghchi amesema “haiwezekani kulitisha taifa la Iran,” na kwamba Rais wa Marekani anapaswa kuzungumza na wananchi wa Iran kwa heshima.

Aidha ametangaza kuwa Lango Bahari la Hormuz “liko wazi kikamilifu,” na limefungwa tu kwa wale wanaoshiriki kwenye vita dhidi ya Iran.

Halikadhalika amesema hatua zote muhimu zimechukuliwa ili kuhakikisha meli za mataifa rafiki zinapita bila wasiwasi.

Araghchi ameongeza kuwa Lango Bahari la Hormuz linaweza kuwa “njia ya amani,” na maamuzi juu ya suala hilo yako mikononi mwa nchi zote za pwani za eneo hilo.

Ameonya pia kuwa Iran “iko tayari kwa aina yoyote ya mapambano ya nchi kavu,” huku akibainisha kuwa anataraji maadui “hawatakosoa katika hesabu zao.”