Lango-Bahari la Hormuz liko chini ya udhibiti kamili wa IRGC
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran (IRGC) limetangaza kuwa Lango-Bahari la Hormuz sasa liko chini ya udhibiti kamili wa vikosi vyake vya majini, huku likitoa maelezo ya mfululizo wa operesheni za makombora na ndege zisizo na rubani dhidi ya malengo ya Marekani na Israel katika maeneo mbalimbali ya kanda.
Katika taarifa yake, IRGC imeongeza kuwa tathmini zinaonyesha kuwa nguvu ya mashambulizi ya ndege zisizo na rubani na makombora ya Iran kuelekea maeneo ya kati ya Israel na sehemu mbalimbali za Asia Magharibi inapingana na madai ya Tel Aviv na Washington kwamba mashambulizi hayo yamepungua kwa asilimia 90.
IRGC imesema kuwa vikosi vyake vya majini tangu alfajiri ya tarehe 1 Aprili vimetekeleza operesheni kadhaa kama sehemu ya wimbi la 89 la Operesheni Ahadi ya Kweli 4, kwa kutumia mchanganyiko wa makombora ya balestiki na ya masafa marefu aina ya Qadeer pamoja na ndege za mashambulizi zisizo na rubani, kwa lengo la kuharibu ngome muhimu za kijeshi za Marekani na Israel.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, katika shambulio la kwanza mifumo miwili ya rada za tahadhari ya mapema za ulinzi wa anga zinazotumiwa na vikosi vya jeshi la Marekani na zilizokuwa zimewekwa kwenye miundombinu ya baharini katika maji na visiwa vya Falme za Kiarabu (UAE) zimeharibiwa kwa usahihi mkubwa.
Taarifa hiyo pia imesema kuwa meli ya kubeba mafuta ya “utawala haramu wa Israel,” iliyotambuliwa kwa jina la “Aqua 1,” imelengwa kwa usahihi katika sehemu ya kati ya Ghuba ya Uajemi, na imeripotiwa kushika moto kufuatia shambulio la kombora.
Kwa mujibu wa IRGC, eneo lililofichwa la mkusanyiko wa wanajeshi wa Marekani nje ya mpaka wa kituo cha Kikosi cha Tano cha Majini cha Marekani nchini Bahrain limeshambuliwa kwa idadi kubwa ya ndege zisizo na rubani pamoja na makombora kadhaa ya balestiki. Ripoti zinaonyesha kuwa maafisa kadhaa waandamizi wa jeshi la majini la Marekani walihamishiwa hospitali mjini Manama baada ya shambulio hilo. Aidha magari mengi ya kubeba wagonjwa na maiti yalionekana katika eneo hilo.
IRGC imesema kituo cha maandalizi ya helikopta aina ya Chinook pamoja na maghala ya kuhifadhi zana za kijeshi katika kambi ya Al‑Udeiri vimeshambuliwa kwa kutumia makombora ya balestiki na ndege zisizo na rubani.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa mawimbi kadhaa ya ndege za mashambulizi zisizo na rubani yalirushwa kuelekea kundi la manowari ya kubeba ndege ya Marekani, USS Abraham Lincoln, katika sehemu ya kaskazini ya Bahari ya Hindi. Kwa mujibu wa picha za satelaiti na nyaraka za ufuatiliaji, meli hizo za kivita za Marekani zilirudi nyuma kutoka nafasi ya awali na kuelekea ndani zaidi ya bahari.
Vilevile, IRGC ilinukuu vyanzo vya kijasusi vikisema kuwa shambulio la awali la vikosi vyake vya majini dhidi ya mkusanyiko wa maafisa wa Marekani katika Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) limesababisha vifo vilivyothibitishwa vya maafisa 37 na majeruhi kadhaa, ambao baadaye walihamishiwa hospitalini.
Mwisho, IRGC imesisitiza kuwa Lango-Bahari la Hormuz linaendelea kubaki chini ya udhibiti kamili wa vikosi vyake vya majini, na ikasisitiza kuwa njia hiyo muhimu ya maji haitafunguliwa tena kwa ajili ya “maonyesho ya kisiasa yasiyo na maana” ya rais wa Marekani dhidi ya taifa la Iran.