Iran: Hujuma dhidi ya madaraja ni uhalifu wa kivita
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i137778-iran_hujuma_dhidi_ya_madaraja_ni_uhalifu_wa_kivita
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani vikali Marekani na utawala wa Israel kwa kutekeleza “uhalifu wa kivita wa kigaidi wa mtindo wa Daesh” wakati wa vita vyao vya kichokozi vinavyoendelea dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu, akisema maadui hao wawili hawatapata nguvu kwa kuharibu madaraja makubwa nchini Iran.
(last modified 2026-04-04T07:50:49+00:00 )
Apr 04, 2026 03:18 UTC
  • Daraja a B1 ambalo limelengwa na kuharibiwa kwa mabomu ya Marekani na Israel
    Daraja a B1 ambalo limelengwa na kuharibiwa kwa mabomu ya Marekani na Israel

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani vikali Marekani na utawala wa Israel kwa kutekeleza “uhalifu wa kivita wa kigaidi wa mtindo wa Daesh” wakati wa vita vyao vya kichokozi vinavyoendelea dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu, akisema maadui hao wawili hawatapata nguvu kwa kuharibu madaraja makubwa nchini Iran.

Esmaeil Baghaei ameandika kwenye akaunti yake ya X kwamba, “Kuharibu madaraja makubwa, yanayosimama kwa fahari kama ushahidi wa ustadi, kujitolea na juhudi zisizochoka za wahandisi na wafanyakazi wa Iran, hakuwafanyi wavamizi kuwa na nguvu.”

Ameongeza kuwa ni “ukweli usiopingika” kwamba uhalifu huo wa kivita wa kigaidi unaofanana na vitendo vya kundi la kigaidi la Daesh, pamoja na mashambulizi mengine dhidi ya miundombinu muhimu ya Iran, unalenga kufikia lengo lao kuu la kuiangamiza Iran.

Msemaji huyo wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesisitiza kuwa tawala za Marekani na Israel zimekuwa zikifuatilia “bila kuchoka” lengo hilo kwa karibu miongo mitano kupitia mashinikizo ya kisiasa, kampeni za kuchafua jina, vikwazo vya kiuchumi, pamoja na mauaji ya wanasayansi na wataalamu bora wa Iran.

Baghaei amebainisha kuwa, pamoja na kuwepo kwa njama hizo, Iran leo imesimama imara zaidi, kwa fahari zaidi na kwa nguvu zaidi kuliko wakati wowote mwingine.

Kauli hiyo imekuja wakati uvamizi haramu wa Marekani na Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ukiendelea, ambapo miundombinu ya kiraia imekuwa ikilengwa mara kwa mara kwa kukiukwa wazi sheria za kimataifa.

Siku ya Alhamisi, Marekani na Israel zilifanya mashambulizi mawili dhidi ya Daraja la B1 la Karaj — moja ya madaraja marefu zaidi Asia Magharibi. Daraja hilo linatambuliwa kuwa mojawapo ya mafanikio makubwa ya uhandisi wa madaraja nchini Iran katika miaka ya karibuni.

Katika ujumbe aliouchapisha kwenye X siku ya Alhamisi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi alisema mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya miundombinu ya kiraia, ikiwemo madaraja ambayo bado hayajakamilika, hayatavunja azma ya Jamhuri ya Kiislamu. Alieleza mashambulizi hayo kuwa ishara ya wazi ya kushindwa na kuporomoka kwa maadili ya wavamizi.

Araghchi ameandika: “Kulenga miundombinu ya kiraia, yakiwemo madaraja ambayo hayajakamilika, hakutawalazimisha Wairani kujisalimisha. Kunadhihirisha tu kushindwa na kuporomoka kwa maadili ya adui aliyeko katika mkanganyiko. Kila daraja na kila jengo litajengwa tena kwa nguvu zaidi. Kile ambacho hakitapona kamwe ni uharibifu uliotokea katika hadhi ya Marekani.”

Maafisa wa Iran wameendelea kusema kuwa kulenga miundombinu ya kiraia ni ishara ya kukata tamaa na ni ushahidi wa kushindwa kwa kimkakati. Wamesema kuwa miundombinu yoyote itakayoharibiwa itajengwa upya kwa uimara na azma kubwa zaidi, huku Marekani ikiendelea kupata madhara yasiyoweza kurekebishwa katika hadhi yake ya kimataifa.