Baqaei: Iran Iko tayari kujilinda mkabala wa vitisho vya adui
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i137904-baqaei_iran_iko_tayari_kujilinda_mkabala_wa_vitisho_vya_adui
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesisitiza utayari wa Tehran kujilinda dhidi ya mashambulizi na vitisho vya aina yoyote vya adui.
(last modified 2026-04-23T09:58:21+00:00 )
Apr 23, 2026 09:55 UTC
  • Ismail Baqaei
    Ismail Baqaei

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesisitiza utayari wa Tehran kujilinda dhidi ya mashambulizi na vitisho vya aina yoyote vya adui.

Akijibu swali la waandishi wa habari kuhusu ombi la Mohammad Ishaq Dar, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan, kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Marekani kurefusha muda wa kusitisha mapigano, Ismail Baqaei ameshukuru juhudi na usuluhishi wa Pakistan katika kumaliza vita vya kulazimishwa na kurejesha amani katika eneo la Magharibi mwa Asia, akibainisha kuwa: 

Jamhuri ya Kiislamu haikuanza vita hivyo vya kulazimishwa, na hatua zote za Iran zimechukuliwa kwa mujibu wa haki yake ya asili ya kujilinda dhidi ya uvamizi wa kijeshi wa Marekani na utawala wa kizayuni wa Israel.

Ameongeza kuwa, kwa msingi huo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, huku ikifuatilia kwa makini yanayojiri katika medani za kijeshi na kisiasa, itachukua hatua muhimu na zinazofaa kulinda maslahi na usalama wa taifa. "Vikosi vya ulinzi pia viko macho na tayari kujilinda kwa nguvu zote dhidi ya vitisho na uovu wowote", amesema Baqaei.

 Kuhusu suala la kufuatilia uhalifu na uharibifu uliosababishwa na mashambulizi ya Marekani na utawala wa kizayuni dhidi ya Iran, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje amesema kuwa: 

Jamhuri ya Kiislamu itatumia kila fursa na uwezo wake kuwawajibisha wavamizi, kurejesha haki za Iran, ikiwa ni pamoja na kutekeleza uadilifu kwa wahusika wa uhalifu wa kivita na kudai fidia.

Akijibu swali jingine kuhusu uwezekano wa kufanyika duru nyingine ya mazungumzo na Marekani, Ismail Baqaei amesema: 

Diplomasia ni chombo cha kulinda maslahi na usalama wa taifa; na mara tutakapofikia hitimisho kuwa mazingira yanaruhusu na yana mantiki kwa ajili ya kutumia chombo hicho ili kuhakikisha maslahi na mafanikio ya taifa la Iran na kumzuia adui kutimiza malengo yake mabaya, tutachukua hatua zinazofaa.