Araghchi: Wairani hawapigi magoti mbele ya mashinikizo
-
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Sayyid Abbas Araghchi
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Sayyid Abbas Araghchi, ameonya kuwa Marekani hukimbilia hatua za kijeshi za kiholela hasa pale suluhisho la kidiplomasia linapoonekana kuwa karibu, huku akisisitiza kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitasalimu amri kamwe mbele ya mashinikizo.
Katika ujumbe aliouandika kwenye mtandao wa kijamii wa X siku ya Ijumaa, Araghchi amesema:
“Kila mara suluhisho la kidiplomasia linapokuwa mezani, Marekani huchagua kuingia katika mchezo wa kijeshi usio na busara. Je, hii ni mbinu duni ya kuongeza mashinikizo? Au ni matokeo ya mpotoshaji ambaye tena amemuingiza rais wa Marekani katika kinamasi kingine?”
Araghchi aidha ameongeza kuwa: “Sababu iwe yoyote ile, matokeo yake ni yale yale: Wairani hawapigi magoti mbele ya mashinikizo kamwe, na diplomasia ndiyo huwa mhanga daima.”
Kauli za waziri huyo zimekuja baada ya Bandari ya Bahman katika Kisiwa cha Qeshm nchini Iran kushambuliwa usiku wa kuamkia Ijumaa, wakati wa mapambano makali kati ya majeshi ya Iran na vikosi vya maadui vilivyokuwa vikifanya operesheni karibu na Mlango wa Bahari wa Hormuz.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Fars la Iran, sehemu za eneo la kibiashara katika bandari muhimu ya Bahman kwenye Kisiwa cha Qeshm zililengwa na kuharibiwa kwa kiasi wakati wa mapambano hayo.
Tukio hilo lilijiri wakati wanajeshi wa Iran walipokuwa wakijibu kwa uthabiti hatua za uhasama katika njia hiyo ya kimkakati ya baharini, na kuwalazimisha washambuliaji kurudi nyuma baada ya kupata hasara.
Katika sehemu nyingine ya matamshi yake, Araghchi amekosoa taarifa za vyombo vya habari zilizomnukuu afisa mmoja wa Marekani akidai kuwa Iran bado ina “takribani asilimia 75 ya uwezo wake wa kabla ya vita wa makombora.” Araghchi amesema: “CIA imekosea. Hifadhi yetu ya makombora na uwezo wetu wa kuyavurumisha hauko katika asilimia 75 ikilinganishwa na tarehe 28 Februari. Takwimu sahihi ni asilimia 120.”
Amesisitiza kuwa,“Na kuhusu utayari wetu wa kuwalinda watu wetu, huo ni asilimia 1,000.”