Pezeshkian: Serikali imejitolea kikamilifu kuboresha uwezo wa Jeshi la Iran
-
Rais Pezeshkian katika kikao na Mkuu wa Jeshi la Iran, Meja Jenerali Amir Hatami
Rais Masoud Pezeshkian amesema serikali yake itatumia “nguvu na rasilimali zote zilizopo” kuimarisha majeshi ya ulinzi huku akisifu majibu ya kijeshi ya Iran kuwa “makini, madhubuti na yanayozuia uchokozi” kufuatia mashambulizi ya hivi karibuni yaliyotekelezwa na tawala za Marekani na Israel.
Katika kikao chake cha Alhamisi na Kamanda Mkuu wa Jeshi la Iran, Meja Jenerali Amir Hatami, Pezeshkian ametambua ujasiri, kujitolea, na uwezo uliooneshwa na Majeshi ya Iran, hasa Jeshi la nchi kavu, katika kukabiliana na vita vya kichokozi vya muungano wa kijeshi wa Marekani na Israel mnamo Februari 28 dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.
Huku akitilia mkazo umuhimu wa umoja wa kitaifa na utayari wa kijeshi wakati mazingira ya eneo yanaendelea kuwa na msukosuko, Rais Pezeshkian ameisifu pia mipangilio ya majeshi kwa majibu yao “ya busara, yenye uwezo na ya kuzuia adui” kufuatia hatua za uhasama zilizochukuliwa na maadui.
Amesema: “Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran lina misingi ya imani, liko karibu na wananchi na ni la kizalendo na limeonesha uthabiti wa ulinzi wa nchi kupitia utayari wa juu wa kivita, uwezo wa kukusanya taarifa za adui, mshikamano wa amri na uwezo madhubuti wa kupambana. Halikuruhusu maadui kutekeleza nia zao ovu dhidi ya taifa la Iran.”
Rais Pezeshkian amesema kuwa mchango wa Jeshi katika kulinda usalama wa taifa, kutetea mipaka ya nchi na kuimarisha uwezo wa kuzuia uvamizi ni “muhimu na wa kimkakati.”
Rais amesisitiza ulazima wa kuendeleza juhudi za kuimarisha uwezo wa ulinzi wa taifa na kuongeza utayari wa kijeshi wa majeshi yote.
Amesema serikali “inasimama bega kwa bega na Majeshi, ikitumia uwezo wake wote kuunga mkono mipango ya kimkakati ya kuongeza nguvu ya ulinzi, kuboresha vifaa, kuimarisha miundombinu ya operesheni na kukuza uwezo wa kuzuia adui.”
Rais Pezeshkian pia amesisitiza umuhimu wa uratibu wa karibu kati ya wizara na taasisi za serikali na Majeshi, kutokana na hali nyeti ya eneo.
Katika kikao hicho, Kamanda Mkuu wa Jeshi la Iran, Meja Jenerali Amir Hatami amewasilisha taarifa kuhusu hali ya operesheni, hatua za ulinzi na majukumu yanayotekelezwa na Jeshi katika kukabiliana na uvamizi na mienendo hasimu.
Pia alifafanua baadhi ya operesheni za jeshi wakati wa wa vita vya hivi karibuni vya siku 40, akisisitiza utayari wa juu wa vitengo mbalimbali vya Jeshi katika nyanja zote.
Jenerali Hatami amewasilisha pia ripoti ya hatua za marekebisho, uimarishaji na kuboresha uwezo wa kijeshi zilizochukuliwa wakati wa kipindi cha kusitishwa kwa mapigano.