Pezeshkian: Iran iko tayari kuihakikishia dunia kwamba haifuatilii silaha za nyuklia
-
Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian
Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, amesema Jamhuri ya Kiislamu iko tayari kuihakikishia jamii ya kimataifa kwamba haifuatilii silaha za nyuklia.
Akizungumza Jumapili alipotembelea Shirika la Utangazaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (IRIB), Rais Pezeshkian alisema Tehran bado inafungamana na diplomasia na utulivu wa kikanda.
Rais amesema kwamba Israel, si Iran, ndiyo chanzo kikuu cha vita na ukosefu wa usalama katika Asia Magharibi.
"Tuko tayari kuihakikishia dunia kwamba hatufuatilii silaha za nyuklia na wala hatutaki machafuko katika eneo hili," amesema Rais Pezeshkian.
"Ni utawala wa Israel unaotumia kila fursa kuendeleza vita na hali ya ukosefu wa amani."
Hata hivyo, Rais Pezeshkian amesisitiza kwamba timu ya Iran katika mazungumzo "hitalegeza kamba kamwe kwenye suala la hadhi na heshima ya taifa."
Tehran inasisitiza haki yake ya kisheria chini ya Mkataba wa Kutoeneza Silaha za Nyuklia (NPT) ya kuendeleza teknolojia ya nyuklia kwa ajili ya uzalishaji wa nishati, utafiti wa kimatibabu na maendeleo ya kisayansi.
Hata hivyo, Marekani na washirika wake wanaishutumu Iran kuwa inafanya jitihada za kupata uwezo wa kiufundi wa kutengeneza silaha za nyuklia.
Tehran imetangaza mara kwa mara kwamba haina nia ya kutengeneza silaha za nyuklia kwa hali yoyote ile.
Matamshi ya Rais Pezeshkian yanakuja huku Iran na Marekani zikiripotiwa kukaribia kukamilisha mkataba wa makubaliano wenye vipengee 14 unaolenga kukomesha vita vya kulazimishwa na kupunguza mvutano katika eneo la Magharibi mwa Asia.