Abdollahian: Aleppo inaelekea kusafika kutokana na uepo wa makundi ya kigaidi
Hossein Amir-Abdollahian, msaidizi maalumu wa Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (bunge), katika masuala ya kimataifa, amesema kuwa hivi sasa mji wa Aleppo, kaskazini mwa Syria unaelea kusafika kutokana na uepo wa makundi ya kigaidi na kitakfiri.
Abdollahian amesema kuwa, mafanikio makubwa ya hivi karibuni ya jeshi la Syria kwa kushirikiana na wananchi katika operesheni za kuusafisha mji wa Aleppo, ni hatua kubwa sana katika njia ya kupambana na ugaidi. Amefafanua kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itaendelea kutoa misaada ya ushauri wa kilojestiki kwa serikali za Iraq, Syria na eneo zima la Mashariki ya Kati katika vita vya kupambana na ugaidi.
Msaidizi maalumu wa Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran, katika masuala ya kimataifa, ameongeza kuwa, ni suala lisilo na shaka kwamba hatimaye magaidi hawatokuwa na nafasi tena katika Mashariki ya Kati. Jumatatu iliyopita, Rami Abdulrahman, kiongozi wa kundi la upinzani nchini Syria na lenye makao yake mjini London, Uingereza alitangaza kuwa, makundi ya wabeba silaha na wapinzani wa serikali ya Damascus, wamepoteza theluthi moja ya mashariki mwa mji wa Aleppo.
Aliongeza kuwa, huko ni kushindwa kukubwa kulikowakuta wapinzani wa serikali tangu mwaka 2012. Hii ni katika hali ambayo baadhi ya duru za makundi ya kigaidi na wapinzani wa serikali ya Syria zimekiri kuwa, wapiganaji wao wamepoteza kikamilifu udhibiti wa eneo la kaskazini mashariki mwa Aleppo na kutwaliwa na jeshi la nchi hiyo.