Kiongozi Muadhamu: Adui anafanya njama za kujipenyeza kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni nchini Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i21388-kiongozi_muadhamu_adui_anafanya_njama_za_kujipenyeza_kisiasa_kiuchumi_kiutamaduni_nchini_iran
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, moja ya malengo makuu ya adui ni kujipenyeza kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni nchini Iran na anawalenga zaidi vijana na mabarobaro wa taifa hili la Kiislamu.
(last modified 2024-06-10T09:25:34+00:00 )
Dec 14, 2016 04:29 UTC
  • Kiongozi Muadhamu: Adui anafanya njama za kujipenyeza kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni nchini Iran

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, moja ya malengo makuu ya adui ni kujipenyeza kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni nchini Iran na anawalenga zaidi vijana na mabarobaro wa taifa hili la Kiislamu.

Ayatullahil Udhma Khamenei alisema hayo jana wakati akihutubia sherehe za kubaleghe na kubeba majukumu ya kidini za wanafunzi elfu mbili wa kiume wa Shule za Msingi za mkoa wa Tehran na kuongeza kuwa, mabarobaro ambao ni watoto wa taifa la Iran leo hii, kesho watakuwa watu wazima na viongozi wa nchi, hivyo wana jukumu la kushiriki vilivyo katika minasaba na mijumuiko mbalimbali ili kujiwekea kinga ya njama kama hizo za adui.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aidha amesema, kipindi cha kubaleghe mtu ni wakati muhimu sana ambao inabidi utumiwe vizuri kumfanya kijana abaleghe kimaanawi na kuongeza kuwa, siri ya maendeleo ya mtu binafsi na ya kijamii ni kulindwa uhusiano baina ya mtu huyo na Mwenyezi Mungu na kwamba kosa kubwa linalofanywa na ustaarabu wa Magharibi ambao hivi sasa unazidi kutoweka na kusambaratika, ni kujiweka kwake mbali na Mwenyezi Mungu.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika mkutano na wanafunzi wa shule za msingi za mkoa wa Tehran

 

Ayatullahil Udhma Khamenei amewataka vijana na mabarobaro kuwafanya mashahidi wa njia ya haki kuwa kigezo chao na kuwakumbusha kwa kuwaambia: Vijana wetu wengi azizi waliouawa kwenye njia ya kulinda uhuru wa taifa lao na maslahi ya nchi yao kwa lengo la kuondoa shari ya maadui, walijitolea kitu azizi na chenye thamani kubwa zaidi kwao, yaani nafsi na roho zao katika njia ya Mwenyezi Mungu.

Amesema, njia bora kabisa ya kuwa karibu na Mwenyezi Mungu ni kushikamana na Sala na kusoma Quráni na kuongeza kuwa, tunapozingatia kwamba mtu huwa anazungumza moja kwa moja na Mwenyezi Mungu Mtukufu na Muweza wakati wa Sala, tutaona kuwa ibada hiyo humtunukia mja nguvu za kutawakali kwa Allah, ushujaa na kujiamini, hivyo dumisheni Sala ya mwanzo wa wakati wake na itekelezeni ibada hiyo kwa mazingatio na shikamaneni na kusoma Quráni na kuzingatia maana na uongofu uliomo ndani yake yake ili mzidi kuwa karibu na Mwenyezi Mungu Mtukufu.