Jan 10, 2017 04:35 UTC
  • Ayatullah Rafsanjani kuzikwa leo, Swala ya maiti inaongozwa na Ayatullah Ali Khamenei

Ofisi ya Hamlashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Kiislamu nchini Iran imetangaza kuwa, mwili wa marehemu Ayatullah Akbar Hashemi Rafsanjani utazikwa leo baada ya Swala ya maiti itakayoongozwa na Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullahil Udhmaa Ali Khamenei.

Taarifa hiyo imesema kuwa, baada ya Swala ya maiti itakayofanyika kwenye msikiti wa Chuo Kikuu cha Tehran asubuhi ya leo, mwili wa marehemu Ayatullah Rafsanjani utazikwa kandokando ya kaburi la mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu, Imam Ruhullah Khomeini katika eneo al Behest Zahraa katika viunga vya mjini Tehran.

Jeneza lenye mwili wa marehemu Ayatullah Rafsanjani

Shughuli ya kusindikiza mwili wa marehemu Ayatullah Rafsanjani inaanza saa nne asubuhi ikiongozwa na Rais Hassan Rouhani, mawaziri wa serikali na maafisa wa ngazi za juu wa jeshi wakifuatiwa na wananchi katika Husainiya ya Jamaran.

Ayatullah Akbar Hashemi Rafsanjani aliyekuwa Mkuu wa Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Kiislamu wa Iran alifariki dunia Jumapili usiku kutokana na matatizo ya moyo.   

Tags