Iran na Zanzibar kuimarisha uhusiano wa pande mbili
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i24145-iran_na_zanzibar_kuimarisha_uhusiano_wa_pande_mbili
Waziri wa Habari, Utamaduni, Michezo na Utalii wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar nchini Tanzania amesema kutangazwa Mash'had kaskazini mashariki mwa Iran kuwa mji mkuu wa kiutamaduni wa ulimwengu wa Kiislamu utaandaa mazingira ya kuimarisha uhusiano wa pande mbili kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Zanzibar.
(last modified 2026-03-27T07:58:19+00:00 )
Jan 24, 2017 04:47 UTC
  • Iran na Zanzibar kuimarisha uhusiano wa pande mbili

Waziri wa Habari, Utamaduni, Michezo na Utalii wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar nchini Tanzania amesema kutangazwa Mash'had kaskazini mashariki mwa Iran kuwa mji mkuu wa kiutamaduni wa ulimwengu wa Kiislamu utaandaa mazingira ya kuimarisha uhusiano wa pande mbili kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Zanzibar.

Rashid Ali Juma, Waziri wa Habari, Utamaduni, Michezo na Utalii wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar amenukuliwa na shirika la habari la IRNA akiyasema hayo jana Jumatatu mjini Mash'had, alipokutana na kufanya mazungumzo na Alireza Rashidian, Gavana wa mkoa wa Khorasan Razavi hapa nchini.

Waziri huyo amefafanua kuwa, uhusiano wa Iran na Zanzibar ni wa jadi, wenye historia pana na wenye thamani na kwamba pande mbili zinafaa kutumia fursa zilizopo na zinazojitokeza kuuimarisha.

Mash'had 2017, mji mkuu wa kiutamaduni wa ulimwengu wa Kiislamu

Kwa upande wake Gavana wa mkoa wa Khorasan Razavi amesema Iran iko mbioni kuimarisha uhusiano wake na madola ya Kiislamu. Ameongeza kuwa, wafanya ziara milioni 27 wa ndani na nje ya nchi huwa wanautembelea mji wa Mash'had kila mwaka.

Alireza Rashidian, Gavana wa mkoa wa Khorasan Razavi hapa nchini amebainisha kuwa, kuna wanafunzi zaidi ya laki 3  wanaosoma katika vyuo vya kidini mkoani humo kwa mujibu madhehebu ya Kishia na Kisunni.

Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Kiislamu (ISESCO), ambalo liliundwa na nchi wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu OIC, liliuteua Mash'had kuwa mji mkuu wa kiutamaduni wa ulimwengu wa Kiislamu.