Zarif: Iran haitaathiriwa na vitisho
Waziri wa Mambo ya Nje ya Iran Mohammad Javad Zarif katika kujibu vitisho vya hivi karibuni vya wakuu wa Marekani ameandika katika ukurasa wake binafsi wa Twitter kuwa: "Iran haitaathiriwa na vitisho".
Zarif alikuwa akijibu madai ya wakuu wa nchi za Magharibi hasa Marekani ambao wamepinga majaribio ya makombora ya balistiki ya Iran na kuongeza kuwa, usalama wa Iran unatokana na uungaji mkono wa wananchi kwa mfumo wa Kiislamu,
Halikadhalika Zarif amesema, kamwe Iran haitakuwa mwanzishaji vita lakini itatumia uwezo wa ndani ya nchi kujihami na kukabiliana vilivyo na maadui.
Siku ya Jumanne pia akizungumza hapa Tehran katika kikao na waandishi habari akiwa ameandamana na waziri wa mambo ya nje ya Ufaransa, Zarif alisema, katika suala la zana zake za kujihami, Iran haitafanya mazungmzo na nchi wala mtu yeyote yule.
Hivi karibuni Michael Flynn, mshauri wa Rais wa Marekani katika masuala ya usalama wa taifa alidai kuwa majaribio ya makombora ya Iran yanakinzana na azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kusema kuwa kuanzia sasa Marekani itafuatilia kwa karibu yanayojiri nchini Iran.
Zarif amesema azimio hilo liliashiria kadhia ya makombora ya balisitiki ambayo yana uwezo wa kubeba silaha za nyuklia katika hali ambayo Iran imetangaza kuwa makombora yake hayana uwezo wa kubeba silaha za nyuklia.