Rouhani: Marekani inajifanya polisi na jaji wa dunia
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i27456-rouhani_marekani_inajifanya_polisi_na_jaji_wa_dunia
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa mara nyingine tena amelaani shambulio la Marekani katika kambi ya jeshi la anga nchini Syria na kusema kuwa, Washington inajifanya polisi na jaji wa dunia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 08, 2017 03:23 UTC
  • Rouhani: Marekani inajifanya polisi na jaji wa dunia

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa mara nyingine tena amelaani shambulio la Marekani katika kambi ya jeshi la anga nchini Syria na kusema kuwa, Washington inajifanya polisi na jaji wa dunia.

Alfajiri ya siku ya Ijumaa, Marekani kwa kutegemea madai yasiyothibitishwa ya eti kutumia serikali ya Syria silaha za kimikali kaskazini magharibi mwa nchi hiyo, ilivurumisha makombora 59 aina ya Tomahawk kutoka katika manuwari yake ya kivita iliyoko kwenye Bahari ya Mediterranean dhidi ya uwanja wa ndege wa Shayrat wa jeshi la Syria huko Homs na kuua raia 9 wakiwemo watoto wadogo wanne na kujeruhi wengine saba.

Rais Rouhani amesema leo Jumamosi hapa mjini Tehran kwamba kuna wajibu wa kuundwa timu ya kimataifa na nchi zisizopendelea upande wowote kwa ajili ya kutafuta ukweli kuhusu madai ya kutumika silaha za kemikali huko Idlib, kaskazini magharibi mwa Syria.

Shayrat

Kituo cha anga cha jeshi la Syria cha Shayrat, Homs

 

Amesema, kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, serikali ya Syria haina silaha za kemikali. Amesema, timu hiyo ya kimataifa ya kutafuta ukweli inapaswa kuundwa na nchi huru zisizopendelea upande wowote bila ya kushirikishwa Marekani ili kuchunguza silaha hizo za kemikali zimetokea wapi hadi kufika huko Idlib.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia amesema, ni nani aliyeipa Marekani haki ya kushambulia nchi huru yenye serikali yake iliyochaguliwa kihalali na wananchi. Amesema, shambulio la Marekani limewafurahisha magaidi na madola yaliyoivamia Syria na kuhoji kwa kusema, kama Wamarekani wanasema kweli kwenye madai yao kuwa wanapambana na ugaidi nchini Syria, kwa nini wanafanya mashambulizi yanayowafurahisha magaidi?