Watu wa Iran wanafuata njia ya ustawi wa Mapinduzi ya Kiislamu
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i27894-watu_wa_iran_wanafuata_njia_ya_ustawi_wa_mapinduzi_ya_kiislamu
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema watu wa Iran wanafuata njia wanayoiona ni yenye maslahi kwao na kwamba wataendelea kufuata njia ya ustawi na ujenzi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 17, 2017 09:09 UTC

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema watu wa Iran wanafuata njia wanayoiona ni yenye maslahi kwao na kwamba wataendelea kufuata njia ya ustawi na ujenzi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Bahram Qassemi ameyasema hayo leo mjini Tehran katika mkutano wa kila wiki na waandishi habari. Akijibu  swali la mwandishi wa Radio Tehran kuhusu madai ya baadhi ya vyombo vya habari vya kigeni kuwa eti kuna mgawanyiko wa pande mbili nchini Iran huku uchaguzi wa rais wa awamu ya 12 ukikaribia, Qasemi amesema: "Taifa la Iran katika kipindi cha miongo kadhaa iliyopita limeonyesha kuwa huwa linafuata kile kilicho na maslahi kwa nchi katika wakati na lahadha muhimu za historia."

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameashiria baadhi ya chokochoko za Marekani katika eneo siku za hivi karibuni na kusema hata bila kutilia maanani mtazamo wa kijeshi wa hatua za Marekani, kile wakuu  wa Washington wanachofanya kinaashiria kuchanganyikiwa katika kukabiliana na matatizo ya ndani ya nchi yao.

Manowari ya kivita ya Marekani ikivurumisha makombora ya Tomahawk kuelekea Syria

Qasemi ameashiria pia mkutano wa Ijumaa baina ya Seneta wa Marekani John McCain na Maryam Rajavi, kinara wa kikundi cha kigaidi cha Munafikin, MKO, huko Tirana mji mkuu wa Albania na kusema: 'Mkutano huo ni kosa ambalo Marekani inapaswa kubeba lawama ya matokeo yake mabaya."

Amesema Marekani imeonyesha kuwa haipati funzo kutokana na makosa yake na sera zake mbovu ambazo zimepelekea kuenea ugaidi katika eneo.