Iran: Kujiondoa US kwenye Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi, hakutauathiri
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema hatua ya Rais Donald Trump wa Marekani ya kuiondoa nchi yake katika makubaliano ya mabadiliko ya tabianchi yaliyofikiwa mjini Paris, Ufaransa mwaka 2015 haitakuwa na taathira yoyote kwenye mkataba huo.
Masoumeh Ebtekar, ambaye pia ni Mkuu wa Shirika la Kulinda Mazingira la Iran amesema makubaliano hayo ni ya kimataifa na kujiondoa kwa nchi moja hakuwezi kuusambaratisha muafaka huo.
Amekumbusha kuwa, nchi 194 zilisaini makubaliano hayo, na kufikia sasa nchi 160 zimejiunga rasmi na mkataba huo unaofahamika kama Mkataba wa Paris hivyo kujondoa nchi moja hakutakuwa na taathira yoyote.
Wakati huo huo, Bahram Qassemi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema hatua ya Marekani kujiondoa kwenye mkataba huo kwa mara nyingine imeuonyesha ulimwengu ni jinsi gani Washington isivyoheshimu makubaliano ya kimataifa.
Amesema mabadiliko ya tabianchi yameisababishia dunia changamoto chungu nzima na kwamba kukabiliana na taathira zake hasi, kunahitajika irada ya kisiasa na ushiriki wa dhati wa nchi zote akisisitiza kuwa, kitendo hicho cha Marekani kitalifanya dola hilo la kibeberu litengwe kimataifa.
Juni Mosi, Trump alitoa tangazo la kuiondoa Marekani katika mkataba huo akisisitiza kuwa, Washington itafanya juhudi za kuanzisha mazungumzo mapya kwa ajili ya kuandika mkataba ulio bora na wenye maslahi kwa Wamarekani.
Hii ni katika hali ambayo, nchi hiyo inaongoza katika uzalishaji wa hewa chafu ya Carbon dioxide ambayo ni moja ya sababu za mabadiliko ya tabianchi duniani.