Uwezo wa kijeshi wa Iran ni wa kuridhisha
Brigedia Jenerali Amir Ali Hajizadeh, Kamanda wa Jeshi la Anga za Karibu na Mbali la Walinzi wa Mapinduzi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, SEPAH, amesema kuwa uwezo wa kijeshi wa hivi sasa wa Iran hauwezi kulinganishwa hata kidogo na wa kipindi cha vita vya miaka minene vya kujitetea kutakatifu na kuongeza kuwa hali hiyo ya kijeshi ni ya kuridhisha.
Akizungumzia uwezo wa makombora na kijeshi wa Iran, Brigedia Jenrali Amir Ali Hajizadeh amesema kwamba hali ya kijeshi ya hivi sasa ya Iran ni ya kuridhisha sana. Amesisitiza kuwa adui hana tena uwezo wa kuchukua kirahisi maamuzi kuhusiana na Iran na kuwa wao wenyewe wanakiri kuwa Iran hivi sasa ni nchi ya saba kwa kuwa na nguvu kubwa ya kijeshi duniani. Nguvu kubwa ya kijeshi kwa ajili ya kulinda usalama wa taifa lolote lile ni sehemu muhimu katika mipango ya kukabiliana na vitisho vya usalama. Hili ni suala muhimu linalozingatiwa na nchi zote za dunia ikiwemo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Kwa maelezo ya Brigedia Amir Ali Hajizadeh, nchi isiyokuwa na nguvu za kiulinzi ni mfano wa mwili iliopungukiwa na seli nyeupe ambapo mtu huathirika na kuangushwa na magonjwa madogo madogo kama mafua. Wakati fulani uwezo wa kiulinzi wa Iran ulikuwa mikononi mwa washauri wa kijeshi wa kigeni wakiwemo Wamarekani ambapo walikuwa wakiathiri pakubwa usalama wa nchi hii, lakini baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hali hiyo ilichukua mkono tofauti kabisa ambapo jukumu la kulinda usalama wa taifa liliwekwa moja kwa moja mikononi mwa Wairani wenyewe.
Kuwa na jeshi lenye nguvu na lililo huru ni nukta muhimu ya uwezo wa kijeshi wa kila nchi na bila shaka Mapinduzi ya Kiislamu yaliipa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran uwezo huo muhimu. Kwa maneno mengine ni kwamba kuwa na nguvu inayodhamini usalama hutimia kwa kuwa na jeshi lenye nguvu kubwa na zana tofauti za kijeshi yakiwemo makombora. Suala hilo muhimu na la kimsingi huiletea nchi nguvu ya kuzuia hujuma kutoka kwa adui na kwa uwezo wake Mwenyezi Mungu na jitihada kubwa zilizofanyika katika uwanja huo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeweza kufikia hatua hiyo ya kuwa na nguvu ya kuzuia hujuma na hivyo kujidhaminia usalama wa kutegemewa.
Kwa kunufaika na teknolojia na vipawa vya ndani ya nchi, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeweza kupiga hatua kubwa katika sekta ya kijeshi na ulinzi suala ambalo limewafanya maadui wasiweze kuchukua hatua yoyote ya kijeshi wanayoitaka dhidi ya mfumo wa Kiislamu. Leo hii hakuna silaha yoyote isiyoweza kutengenezwa na wataalamu wa Kiirani na hali hii inaendelea kuimarika kila siku.
Hivi sasa reda, vituo vya udhibiti wa kamandi, teknokojia ya vita vya eletroniki, mifumo ya makombora mbalimbali ya kisasa iliyo na nguvu kubwa na zana nyingine za vita, zote hizo zinatengenezwa na kudhibitiwa na wataalamu wa Kiirani. Kwa maneno ya Amir Ali Hajizadeh mwenyewe, hivi sasa Iran inajitosheleza kikamilifu katika sekta ya utengeneza wa zana mbalimbali na za kisasa kabisa za anga yakiwemo makombora erevu na ndege zinazoruka bila ya kuwa na rubani. Zana zote hizo muhimu katika sekta ya ulinzi zimeifanya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa nchi yenye taathira kubwa katika matukio ya kisiasa na kijeshika kieneo. Iran ni nchi iliyo huru katika maamuzi yake na hasa ya kisiasa na kijeshi na hapa ndipo unapoanzia uadui usiokoma wa Marekani dhidi ya taifa hili la Kiislamu, ili kulifanya lisiwe na uwezo wa kujibu mapigo ya kijeshi. Uwezo wa makombora ya Iran ndicho kilele cha kudhaminiwa usalama wa kuaminika.
Jibu kali la makombora lililotolewa hivi karibuni na kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu dhidi ya kituo cha magaidi na waungaji mkono wao wa Kisaudia, Kimarekani na Kizayuni huko Syria, magaidi ambao kabla ya hapo walikuwa wametekeleza mashambulio ya kigaidi mjini Tehran tarehe 7 Juni, lilibainisha wazi nguvu ya kijeshi ya Iran na wakati huohuo kutoa ujumbe muhimu kwa maadui wa taifa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Kuhusu jambo hilo, Faisal al-Miqdad, Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Syria alisema siku tatu zilizopita kwamba shambulio hilo la makombora la Iran lilitekelezwa wakati mzuri sana ambapo lililenga mkusanyiko wa magaidi wa Daesh waliokuwa wamekusanyika katika kituo chao huko Dair Ezzor ambapo mbali na kuwalenga magaidi hao lakini pia lilikuwa na ujumbe maalum na wa wazi kwa waungaji mkono wa ugaidi na hasa Marekani, Saudia Arabia na utawala ghasibu wa Israel.