Sep 01, 2017 08:20 UTC
  • Imamu wa Swala ya Idi Tehran: Hija inapaswa kuzingatia matatizo ya Waislamu

Hatibu wa Swala ya Idul Adh'ha iliyoswaliwa mapema leo mjini Tehran amesema kuwa, falsafa ya amali za ibada halisi ya Hija ni kutilia maanani masuala na matatizo ya Ulimwengu wa Kiislamu na mashaka yanayowakumba Waislamu kote duniani.

Ayatullah Muhammad Emami Kashani amesema katika hotuba za Swala ya Idi kwamba, falsafa ya amali za Hija, kwenda kwenye Nyumba ya Mwenyezi Mungu na kukusanyika kwa Waislamu kutoka pembe mbalimbali za dunia huko Makka ni kushughulikia masuala ya Waislamu na kuuzindua Umma kuhusu hali inayotawala dunia ya leo. Amesisitiza kuwa, Waislamu wanapaswa kuzitaka tawala na viongozi wa nchi zao kuimarisha amani, umoja wa Kiislamu na kuzuia mifarakano katika Umma wa Kiislamu. 

Imam wa Swala ya Idi mjini Tehran ameashiria njama zinazofanywa na maadui wa Uislamu, mabeberu wa dunia na Uzayuni wa kimataifa kwa ajili ya kuanzisha vita na umwagaji damu katika maeneo mbalimbali ya dunia na kusema kuwa: Wanafikra wa Kiislamu na mahatibu wa Swala za Ijumaa wanalazimika kutumia ibada ya Hija kueleza hali mbaya ya Palestina, Yemen na Syria na kutilia maanani maslahi ya Waislamu kote duniani. 

Swala ya Idi mjini Tehran

Itakumbukwa kuwa katika ujumbe wake uliosomwa jana kwa mahujaji wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu kwenye jangwa la Arafat, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei pia aliashiria siasa za mfumo wa kibeberu za kutaka kuzusha mifarakano kati ya Waislamu na kusema kuwa, ni wajibu wa viongozi wa nchi za Kiislamu, wasomi na wanafikra wa Kiislamu kuimarisha umoja, kuyazindua mataifa mbalimbali na kusitisha mara moja maafa machungu yanayowasibu Waislamu.   

Tags